December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku 365 za Rais Samia, na mafanikio katika sekta mbalimbali Ilemela

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Katika siku 365 za Rais Samia Suluhu Hassan,amefanikiwa kufanya masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika Wilaya ya Ilemela ikiwemo uboreshaji was sekta ya afya,elimu,maji na mengineyo.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho,katika hafla ya maadhimisho ya siku 365 za Rais madarakani kwa Wilaya ya Ilemela,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masalla,alisema ndani ya mwaka mmoja walipokea zaidi ya bilioni 45 za miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hawajapata changamoto ya ubadhirifu wa fedha hizo za umma,wanazisimamia kwa weledi na umakini ili zitumike vizuri.

Masalla amesema, katika sekta ya afya Ilemela imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuongeza dawa na vifaa tiba pamoja na ongezeko la kituo cha afya Kayenze na ujenzi wa zahanati 3 za Lumala, Nyamadoke na Masemele.

“Katika kipindi hicho Wilaya ilipokea fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kayenze ambacho kimejengwa kwa kiasi cha milioni 500 fedha zinazotokana na tozo ya miamala,vituo vya afya vya Buzuruga na Karume vimeboreshwa ,zahanati tatu zinajengwa kwa kiasi cha milioni 150 ambapo hadi kufikia Mei,mwaka kuu zitamilika na kuwahudumia wananchi,dawa na vifa tiba zinapatikana baada ya MSD kuzisambaza kwa wakati,”amesema Masalla.

Masalla amesema mafanikio mengine katika Wilaya hiyo ndani ya mwaka mmoja imefanyika kazi kubwa kwenye sekta ya elimu ambapo madarasa 97 ya shule za sekondari yamejengwa kwa gharama ya bilioni 1.94 na kusaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani na mazingira yameboreshwa na kuwavutia wanafunzi.

Huku madawati zaidi ya 4000 yakitengenezwa pia Wilaya imepokea kiasi cha milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Buzuruga.

Pia amesema,,licha ya wilaya hiyo kuwa karibu na Ziwa Victoria ina changamoto ya maji hivyo zaidi ya bilioni 12 zimetengwa kuitatua ambapo miundombinu ya maji inajengwa na kuifanya kero ya maji kuwa historia.

Aidha ameeleza kuwa, ili kujenga uchumi fungani na jumuishi,Serikali ya awamu ya sita imekamilisha mradi wa kimkakati wa stendi mpya ya Mabasi na Maegesho ya Malori Nyam’hongolo uliogharimu kiasi cha bilioni 26.6 utakaohudumia mabasi 200 kwa wakati mmoja huku maegesho yakihudumia malori 300 kwa siku,utawainua wananchi wa Ilemela kiuchumi na kijamii kwa kufanya shughuli mbalimbali.

“Tunapoadhimisha siku 365 za Rais Samia hatuwezi kusahau miundombinu hii ya kimkakati inayolenga kurahisisha maisha,kujenga na kuinua uchumi wa wananchi wa Ilemela,mradi utakuwa na kila aina ya shughuli muhimu za kijamii na kibinadamu,”amesema Masalla.

Vilevile amesema,fedha za miradi hiyo zinatokana na jitihada za Rais Samia,wanamtakia kila la kheri,amewaletea Ilemela kufanya kazi za Watanzania na wataendelea kufanya vizuri,miundombinu ya barabara amewaongezea fedha nyingi kutoka bajeti ya bilioni 1.2 hadi bilioni 3.5 pia watafunga taa kwenye barabara Airport na Buswelu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amesema,wanaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kumtua mama ndoo kichwani ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuibua miradi ya maji Ilemela.

Naye Mstahiki Meya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga,amesema wao kama iBaraza la Madiwani kwa umoja wao wataendelea kusimamia matumizi bora ya fedha zote zinazoingia kutoka serikali kuu na kwingineko kwa manufaa ya Halmashauri na zile zinazopatikana kutokana na mapato ya ndani kutoka vyanzo mbalimbali lengo ni fedha zote zitumike kama zilivyopangwa ili zilete tija kwao wana Ilemela.

Mwakilishi wa wajasiriamali, Agnes Noel,amesema uwajibikaji wa serikali ya awamu ya sita umesaidia kuboreshwa kwa barabara ya Jiwe Kuu Bwiru,umewanusuru na kuwaokoa wanawake kutoharibika ujauzito pia wajasiriamali watanufaika kwa mikopo,pia stendi ya Nyam’hongolo.

Mwakilishi wa Machinga Modest Simfukwe,amesema ndani ya mwaka mmoja kundi hilo limetambuliwa na kurasimishwa, limejengewa mazingira mazuri ya kufanya biashara na tayari serikali imeleta milioni 500 za kuwajengea masoko ya kisasa ili kuboresha biashara zao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku 365 ya Rais Samia madarakani,kwa Wilaya ya Ilemela iliofanyika wilayani humo mkoani Mwanza. (Picha na Judith Ferdinand)