Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Morogoro
KITUO cha kuendeleza kilimo nyanda za kusini mwa Tanzania (SAGCOT) imeingia makubaliano na Sekta Binafsi pamoja na Asasi zisizo za kiserikali kuongeza uzalishaji wa mazao katika mkoa wa Morogoro sambamba na kukuza kilimo biashara kinachozingatia utunzaji wa mazingira na rasilimali zake.
Akizungumza wakati kufunga kikao cha siku mbili kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana SAGCOT pamoja na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo uliofanyika jana mjini Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela amesema makubaliano haya yataleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Makubaliano haya ni maazimio ya kikao chetu hivyo kila mdau kwa nafasi yake awajibike ili kasi ya uzalishaji mazao uongezeke na kuchangia kipato kwa wananchi na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla,” alisema Bw.Shigela
Ameeleza baadhi ya maazimo ikiwa ni pamoja na marekebisho ya sera,kanuni na sheria na ujenzi wa miundombinu kwa upande wa Serikali itawajibika ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Aidha kwa upande wa Sekta binafsi itawajibika kakuhakikisha inakuza ajira hususani kwa vijana, mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha, kutafuta masoko ya mazao yanayozalishwa na teknolojia za kisasa katika kuboresha uzalishaji mazao ili kukuza uchumi wa nchi.
“Tumekubaliana kuwa asasi zisizo za kiserikali zinawajibika katika uwezeshaji wa kusambaa kwa teknolojia stahiki kwa wakulima, kutoa elimu kwa wakulima ili kuwajengea uwezo sambamba na elimu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira,” amesema Shigela
Aidha, Shigela aliwataka wakuu wa wilaya wote katika mkoa wake washirikiane na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi zinafanyiwa kazi ili malengo yaliyoadhimiwa yanatekeleza kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuifanya morogoro kuwa kapu la chakula nchini.
“Mkoa wetu umebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao mbalimbali tutumie fursa hii kuhakikisha kilimo, mifugo na uvuvi vinafanyika kwa tija ili kuongeza uzalishaji zaidi wa mazao,” alisema Shigela
Kwa upande wake Meneja wa SAGCOT, Kongani ya Kilombero, John Nakei amesema makubaliano hayo yamejikita kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya Serikali,Sekta binafsi na Asasi zisizo za Serikali ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
“Lengo kubwa ni kumwezesha mkulima mdogo kufanya kilimo cha kisasa kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambacho kitamletea tija kwenye uzalishaji na kupelekea kukuza uchumi wake na kufikia maendeleo sambamba na utunzaji mazingira,” amesema Nakei
Naye Mkuu wa idara ya mahusiano Kiwanda cha Sukari Kilombero, Ephrahim Mafuru amesema maazimio yaliyowekwa yatachangia katika kuongeza uzalishaji mazao ambayo ni malighafi katika viwanda jambo linalomhakikisha mkulima soko la uhakika la mazao yake.
“Naishukuru sana SAGCOT kwa namna inavyotupambania katika kuhakikisha viwanda vinapata malighafi zenye ubora kwa kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija huku wakizingatia ubora,” amesema Mafuru.
Kikao hicho cha siku mbili kimeratibiwa na SAGCOT kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuwakutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo pamoja na taasisi binafsi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi