November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC yamzawadia tuzo Dkt.Kijo Bisimba kwa kupigania haki za binadamu

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THDRC)umempongeza na kumpa tuzo ya maisha Mkurugenzi Mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),Dkt Hellen Kijo Bisimba kwa kufanya kazi za haki za binadamu.

Akitoa tuzo hiyo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani,Mratibu wa Mtandao huo,Onesmo Olengurumwa amesema wametoa tuzo hiyo kwa Dkt.Bisimba kwa sababu ni mwanamke  aliyesimama katika utetezi wa haki za binadamu.

Amesema historia ya Dkt.Bisimba ya utetezi wa haki za binadamu kwa miaka mingi hivyo wameona ni vema kumpatia tuzo ya maisha ya mtetezi wa haki za binadamu.

” Dkt. Bisimba amekuwa mstari wa mbele ni miongoni mwa mwanamke wa pekee kwa utetezi wa haki za binadamu hapa nchini tangu mwaka wa 1990 amefanya mambo mengi makubwa katika kupigania masuala ya haki za kisiasa, demokrasia, haki za ardhi, makundi maalum, “alisema na kuongeza

“Licha ya kupata changamoto zote katika utetezi wa haki za binadamu lakini hakukata tamaa tukasema tumtambue mchango wake katika jamii,”amesema

Amesema kikubwa licha ya kustaafu uongozi katika kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ameendelea kusimamia na kutetea haki za binadamu.

Kwa upande wake,Dkt.Bisimba
ameshukuru kwa kupata tuzo hiyo na kueleza kuwa alikuwa anajitolea hakutegemea kama angepatiwa zawadi hiyo.

“Hii tuzo nimeambiwa ni ya maisha ya utetezi wa haki za binadamu kwamba nikiwa hai msije mkafikiri nitaacha  kutetea haki za binadamu.”amesema na kuongeza

“Kila mtu anaweza kuwa mtetezi pale unapoona kuna mwenzako anavunjiwa haki zake,tusiogope kutetea watu wanapovunjiwa haki zao,”amesema