November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yapiga hatua mapambano dhidi ya UKIMWI

 Na. Mwandishi Wetu-

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dodoma

Serikali imesema imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini kwa kutelekeza programu mbalimbali za utoaji elimu na huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma akitoa taarifa ya mafanikio ya Ofisi yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Pindi amesema  miongoni mwa hatua kubwa zilizopigwa na serikali ni pamoja na kudhibiti vifo vitokanavyo na UKIMWI ambapo vimepungua  kwa asilimia 50  kutoka 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2021.

 “Katika kipindi  cha mwaka mmoja mafanikio ya Serikali yaliyoshuhudiwa katika eneo hili ni kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU katika jamii ikiwemo maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kushuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2021,”alisema Mhe. Pindi.

Akibainisha mafanikio mengine katika mapambano dhidi ya UKIMWI alisema kwamba ni kushuka kwa kiwango cha unyanyapaa katika jamii kutoka asilimia 28 mwaka 2013 hadi asilimia 5.5 mwaka 2021, na  Nchi kuwa katika  hatua nzuri za kufikia malengo ya Kidunia ya Tisini Tatu (90-90-90) mwaka 2020 na Tisini na Tano Tatu (95-95-95) mwaka 2025.

“WAVIU wanaofahamu hali zao za mambukizi ni asilimia 83, WAVIU wanaofahamu hali zao za mambukizi na wapo kwenye matibabu ni asilimia 98 na WAVIU waliopo kwenye matibabu na wamefubaza VVU ni asilimia 92,”alieleza Waziri Pindi.

Pia akitaja mafanikio mengine ya Serikali ya Awamu ya Sita alifafanua kuwa ni pamoja na Uzinduzi wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali ambao unaendelea na ukitarajiwa kukamilika mwaka 2022/23.

“Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara zenye urefu wa KM 51.2 katika mji huo zinajengwa kwa kiwango cha lami. Katika mwaka 2021/22 jumla ya Shilingi bilioni 300 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi na Miundombinu,”Alibainisha.

Kuhusu mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya Mhe. Pindi alisema Kliniki sita za tiba ya Methadone zimeanzishwa katika mikoa ya  Songwe,Arusha na  zingine nne Jijini Dar es Salaam hivyo kufanya kliniki hizo kufikia 15  Nchi nzima zinazohudumia  zaidi ya waathirika 10,600 wa dawa za Kulevya kila siku.

“Serikali imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya Methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake na ili kuhakikisha wanainuka kiuchumi vijana 200 wanaopatiwa matibabu kwenye kliniki za Methadone wamejumuishwa katika Programu ya Kukuza Ujuzi kupitia Vyuo vya VETA ili kuwajengea ujuzi wa kufanya kazi za kiuchumi,” Alifafanua Mhe. Pindi.

Aidha alieleza kwamba Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa  njia mbalimbali ambapo vilabu vya kupinga dawa za kulevya vimeanzishwa  shuleni na walimu 66 wamepatiwa elimu  ili kuwawezesha kusimamia klabu hizo, vyuoni na elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya ambapo inakadiliwa zaidi ya wananchi millioni 10 wamefikiwa na elimu hiyo.

“Serikali imeendelea kuhakikisha inadhibiti matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kuwanusuru wananchi wake kuathirika na dawa hizi kwahiyo hatua hii ya Serikali  imesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia wimbi la vijana kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa hizo,” 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wake kuhusu mafanikio ya Ofisi yake kwa Kipindi cha mwaka mmoa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan uliofanyika tarehe 9 Machi, 2022 katika Ofisi zake zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Kaspar Mmuya (kushoto) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa Bw.Batholomeo Jungu (kulia) wakifuatilia mkutano huo.
Mkuu wa kitengo cha Mawasilino Ofisi ya Waziri Mkuu Augustino Tendwa akiongoza mkutano wa waandishi wa habari kuhusu maafanikio ya ofisi hiyo katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na Mhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Saudeni Ananic alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Awamu ya pili wa jengo la Ofisi yake lililopo Mji wa Serikali Mtumba mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Naibu Katibu Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Kaspar Mmuya akifafanua jambo kwa wandishi wa habari kuhusu masuala ya uratibu wa shughuli za Serikali wakati wakikagua maendeleo ya ujenzi wa Majengo ya ofisi hiyo kwa Awamu ya Pili.