November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkenda asisitiza kutowaficha ndani watoto wenye Ulemavu

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

SERIKALI imejipanga kuhakikisha kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma zote stahiki ikiwemo elimu kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo juzi ,mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye shule ya sekondari Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam.

Prof Mkenda ametoa mwito kwa watanzania wote hususani wazazi kutowawaficha ndani watoto wenye mahitaji maalumu badala yake wawapeleke shule ili waweze kupata elimu.

“Katika uongozi wa Rais wetu Mhe Samia Juhudi mbalimbali zinafanyika ili kuendeleza fursa kwa wanafunzi kupata elimu bila kikwazo,” Amesema Prof Mkenda

Amesisitiza kuwa kwa sasa serikali imekamilisha ujenzi wa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Wilaya ya Masasi mkoani Lindi pamoja na Arusha na shule nyingine ambayo ujenzi wake unaendelea mkoani Geita.

Waziri Mkenda amesema kuwa ndani ya mwaka mmoja serikali imejenga vituo shikizi 3000 vya kusomesha watoto ambapo kwa wale wasioweza kuifikia huduma ya elimu wanaweza kufikishiwa popote walipo.

Amesema kuwa tayari kamishna wa elimu Tanzania ametoa muongozo wa namna ya kuwapokea wanafunzi ambao waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali  ili warejee kusoma.

Waziri Mkenda amemuhakikishia Rais Samia kuwa, tayari wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutekeleza maagizo aliyoyatoa kuhusu kupitia upya mitaala ya elimu kwa ajili ya kuongeza ubora wa elimu na pia kuifanya elimu iweze kuakisi mahitaji halisi ya nchi.