Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya
MWENYEKITI wa bodi ya wakurugenzi ya mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) Juma Muhimbi ameonya baadhi ya wadau wa mfuko huo ambao wamekuwa si waaminifu kutokana na kuhujumu mfuko na kusema kuwa tabia hiyo iachwe mara moja .
Muhimbi amesema hayo jana wakati wa mkutano wa wadau wa mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao umefanyika Mkoani mbeya katika ukumbi wa mfuko huo uliopo Jijini hapa.
Aidha Mwenyekiti huyo amesema kuwa tayari baadhi ya wadau wameshafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kufuatia kuhujumu mfuko huo.
Hata hivyo Muhimbi ametoa rai kwa wadau wa mfuko kuacha hiyo tabia na
kwamba bodi yake wataendelea kupiga vita kwa nguvu zote ubadhilifu wa mfuko huo na kwamba kila mtu ana wajibu wa kuwa na nia moja katika kuhakikisha mfuko huo unastawi ili watu wao waendelee kufaidika sasa na vizazi vijavyo.
“Ndugu zangu kuwepo kwa mfuko huu ni manufaa kwa pande zote wakiwemo wanachama na watoa huduma , hivyo itakuwa ni hasara kwetu sote endapo tutaachia mfuko huu ukafa kwa sababu ya ubadhilifu,tuulinde mfuko ili utulinde”amesema Mwenyekiti huyo wa bodi.
Akifafanua zaidi Muhimbi alisema kwamba hivi sasa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kujenga Tanzania ambayo wananchi wake wana uhakika wa kupata huduma za matibabu na ndio maana ya kuweka katika kutekeleza suala la bima ya afya kwa wote.
Akielezea zaidi Mwenyekiti wa bodi huyo , alisema kuwa mpaka sasa asilimia nane (8) ya watanzania ndio wananufaika na huduma za NHIF na kwamba asilimia hiyo bado ni ndogo hasa ukizingatia umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa wananchi .
Naye Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa bima ya afya Taifa (NHIF) Bernard Konga amesema kuwa mfuko huo unakuja na mikakati ya kuongeza wanachama zaidi wa kizazi cha kati ili kuhakikisha kuwa wanajumuishwa kwenye huduma ya afya .
Kwa upande Mwenyekiti wa baraza la wadhamini la wawekezaji wa elimu Tanzania (TAPIE)Mahmoud Mringo ametoa ushauri kwa uongozi wa mfuko wa bima ya afya kuwafikiria wagonjwa wa magonjwa ya kudumu kuwepo kwenye mfuko huo kutokana na matibabu yake kuwa gharama kubwa.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunzi
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu