November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za serikali wazinduliwa

Na David John, TimesMajira Online

JESHI la Polisi kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Amend wamezindua mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za serikali jijini Dar es Salaam.
Mradi huo ujulikanao kama ‘Mahakama ya watoto’ utahusisha utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa zaidi ya wanafunzi 11,000.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi za jeshi hilo zilizopo Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, SACP Wilbroad Mutafungwa alisema mradi huo utatoa kipaumbele kwa shule zenye wanafunzi wenye uhitaji maalum.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) linakadiria kuwa watu takriban 3,700 hufariki kila siku kwa ajali za barabarani duniani kote, huku Afrika ikiwa na idadi kubwa zaidi ya majeruhi watokanao na inaongezeka kila mwaka kutokana na kukua kwa kasi ya maendeleo.

“Nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2021, watu 1,245 walipoteza maisha na wengine 2,023 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani. Taarifa zinaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 56 walipoteza maisha na wengine 65 kujeruhiwa katika ajali hizo.

“Mwaka huu katika kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali nchini, Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani tukishirikiana na Amend tutaendesha mradi huu wa Mahakama ya Watoto ambao utahusisha kutoa elimu na mahojiano maalum ambayo yanafanywa kati ya wanafunzi na madereva watakaobainika kuvunja sheria za usalama barabarani kwenye maeneo ya shule hizo,” amesema Mutafungwa.

Hata hivyo Mutafungwa aliwataja waathirika wakuu wa ajali za barabarani kuwa ni watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na bajaji, watoto wadogo wanaopandisha mshikaki kwenye pikipiki pamoja na madereva wa magari ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani.

Naye Meneja Mkuu wa Amend, Simon Kalolo alisema mradi huo utashirikisha shule 10 za mkoa wa Dar es Salaam zenye uhitaji.

“ kimsingi mafunzo haya yatawasaidia wanafunzi hao kutoa elimu ya usalama barabarani moja kwa moja kwa madereva. Na baada ya kukamilisha mradi huu tutatoa vyeti vya kuwatambua washiriki wote,” amesema Kalolo.

Ameongeza kuwa, mradi wa namna hiyo ulitekelezwa mwaka 2019na 2020 jijini Dar es Salaam na baadae mkoani Tanga mwaka 2021.

“Tuna shule nyingi ambazo serikali imeweka alama maalum lakini wengine hawazifahamu na wengine hawaoni umuhimu wa kuzitumia, kwahiyo kupitia mradhi huu tutawaelimisha,” amesema Kalolo.

.Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Wilbroad Mutafungwa akimkabidhi cheti cha ushirikiano bora wa usalama barabarani,Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali Tanzania la Amend,Saimon Kalolo (kulia)wakati wa uzinduzi wa mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za Serikali za jijini Dar es Salaam ujulikanao kama ‘Mahakama ya Watoto’