November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndalichako apongeza uwekezaji

Na: Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Kilimanjaro

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amepongeza uwekezaji kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) pamoja na Jeshi la Magereza Tanzania kwa hatua nzuri ya ukamilishaji wa kiwanda cha uzalishaji bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd).

Waziri Ndalichako ametoa pongezi hizo Februari 26, 2022 baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kukagua maendeleo ya kiwanda na kuangalia namna ya uzalishaji wa bidhaa.

Alisema kuwa, amefurahishwa na uwekezaji katika kiwanda hicho ambacho kitatoa ajira nyingi kwa vijana pamoja na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa kupitia bidhaa zitakazo kuwa zinazalishwa na kiwanda hicho.

“Kiwanda kimefikia hatua nzuri na Mashine zote zimeshafika, hatua inayoendela ni kuziunganisha mashine hizo ili uzalishaji uendelee kufanyika wanatengeneza. Viatu vinavyotengenezwa hapa ni vizuri na wanatengeneza viatu vyenye mitindo ya aina mbalimbali,” aliema Prof. Ndalichako.

Aliongeza kuwa, uwepo wa Kiwanda cha bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kitachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira nchini mara tu baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho.

“Kiwanda kinauwezo wa kuajiri watu zaidi ya 10,000 ambapo ajira za moja kwa moja ni 3,000 pamoja na ajira zaidi kwa watanzania kutokana na fursa mbalimbali zitakazo kuwepo kiwanda hapo,” alisema

Aidha, Waziri Ndalichako aliwasihi watendaji wa kiwanda hicho kuhakikisha malengo ya uzalishaji katika kiwanda yanazingatiwa ili fedha zilizowekezwa zitumike kwa matokeo yaliyokusudiwa.

Sambamba na hayo amewapongeza Uongozi wa Chuo cha VETA pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) kwa kutoa mafunzo bora kwa vijana ya utengenezaji wa bidhaa za Ngozi, huku akibainisha kuwa vijana wanaotoka katika vyuo hivyo wamekuwa watengenezaji wazuri wa viatu. Hivyo alitoa wito vijana kuchangamkia sekta ya Ngozi kwa kuwa serikali imeanza kuwekeza katika kiwanda cha Ngozi na kutakuwa na uhitaji wa rasilimali watu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro, Mhandisi. Masud Omary ameeleza kuwa menejimenti ya kiwanda hicho imejipanga kuendelea kukuza masoko ya bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo ili kuhamasisha wananchi kununua bidhaa hizo. Pia alieleza juhudi zinazofanywa na kiwanda katika kukuza soko la bidhaa nje ya nchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akiangalia kiatu cha Ngozi alipotembelea kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) kwa lengo la kukagua maendeleo ya kiwanda na kuangalia namna ya uzalishaji wa bidhaa, Februari 26, 2022 Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Wa pili kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro Mhandisi. Masud Omary na Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Festo Fute (wa pili kutoka kulia).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) kwa lengo la kukagua maendeleo ya kiwanda na kuangalia namna ya uzalishaji wa bidhaa, Februari 26, 2022 Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu akichangia jambo wakati wa ziara hiyo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipotembelea kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) Februari 26, 2022 Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro Mhandisi. Masud Omary akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda hicho wakati wa ziara hiyo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipotembelea kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) kwa lengo la kukagua maendeleo ya kiwanda na kuangalia namna ya uzalishaji wa bidhaa, Februari 26, 2022 Moshi, Mkoani Kilimanjaro.