November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watakiwa kuhakikisha jamii inanufaika na uwepo wao

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wadau wanaotekeleza masuala ya kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto nchini wametakiwa kuhakikisha Jamii inanufaika na uwepo wao kwa kuhakikisha jamii inapata elimu ya kuondoka na Vitendo vya Ukatili.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma tarehe Februari 26, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akifungua kikao kazi na Wadau waotekeleza afua za kupambana na vitendo vya ukatili nchini.

Waziri Dkt. Gwajima amesema pamoja na kuwepo Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto yaani (MTAKUWWA) bado changamoto ya vitendo vya ukatili inaendelea hivyo wadau wanatakiwa kuunganisha nguvu katika kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka wadau kushirikiana na Serikali kuamua kukabiliana na changamoto hizo ili kuepuka kuongezeka na wahanga wa vitendo vya ukatili.

“Ni imani yangu kuwa, kikao kazi hiki kitajielekeza kwenye kupata majibu ya kutumia mbinu gani kuzuia ukatili wa majumbani kwa watoto na Wanawake na mbinu gani za kiwanusuru watoto walio wahanga wa ukatili kukimbilia na kufanya kazi Mitaani” amesema Mhe. Gwajima.

Ameongeza kuwa, moja ya changamoto za kuendelea kutokea kwa vitendo vya ukatili ni utendaji hafifu wa Kamati za ulinzi wa Wanawake na Watoto hususani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa pamojana kuwepo kwa Kamati 18,186 nchi nzima.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Mwanaidi Khamis alisema, Ukatili unaofanyika ndani ya Jamii, ndio umekuwa unadhorotesha jitihada za Serikali katika Kusukuma gurudumu la Maendeleo kutokana na watu kukatiliwa, hivyo kitendo cha Mhe. Rais kuanzisha Wizara hii, ni hatua kubwa katika kulipa kipaumbele suala lakutokomeza ukatili.

Awali akizungumza katika kikao kazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto Dkt. Zainab Chaula amesema engo la kikao hicho ni kutaka kujua mikakati gani waliojiwekewa wadau katika kukabiliana na vitendo vya ukatili.

“Vitendo vya ukatili vimeongezeka, wadau tupo wapi, watoto wanalala mtaani, Jamii inatakiwa inufaike na uwepo wa Mashirika haya” Dkt. Chaula

“Kati ya Mashirika elfu 12, ni Mashirika 6000 tu ndiyo yamejitokeza kusema shughuli wanazofanya, hivyo tuliamua kuwa ifikapo tarehe 28 Februari, mwaka huu Mashirika ambayo hayajajitokeza hayatatambuliwa” alisisitiza Dkt. Chaula

Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika linaloshughulikia la Plan International Peter Mwakabwale amemshukuru Waziri kwa kuwakutanisha Wlwadau na kuwapa ushirikiano hivyo wamepata nguvu ya kuhakikisha wanapambana na vitendo vya ukatili kwenye jamii kwa kuhakikisha jamii inapata elimu ya kupambana na vitendo hivyo.

“Tupo wadau wengi tunaotekeleza afua mbalimbali kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto lakini bado kuna changamoto ni muda sasa wa kusimaam pamoja na kuazimia Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto” amesema Peter.

Peter amebainisha jitihada zikizofanyika na wadau ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za MTAKUWWA ngazi zote, kuimarisha huduma za upatikanaji wa Huduma za uzazi na mafunzo kwa Viongozi wa Dini.

Naye Mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamato ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Neema Lugangira amesema kuwa wadau na Serikali wanatakiwa kuona namna ya kuongeza afua ya ukatili wa kijinsia mtandaoni kutokana na wimbi la ukatili huo.

“Wakati umefika wa kutambua tatizo la Afya ya akili, Jamii ielimishwe kuhusu kuzungumza na wataalamu wa ushauri nasaha kuhusu changamoto zao” alisema Mhe. Neema