Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online
Ukatili wa kimtandao ni miongoni mwa ukatili ambao unashamiri kwa kasi katika jamii huku madhara yake yakiwa ni makubwa hususani kwa mabinti na vijana.
Hivyo mwarobaini wa ukatili huo ni wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao huku elimu ikitolewa ya matumizi sahihi ya mtandao ya nini kinachotakiwa kuweka katika kurasa za mitandao na madhara yanayoweza kutokana na mtu kupiga picha zilizo kinyume na maadili.
Akizungumza na majira/ timesmajira kwa njia ya simu Mkurugenzi wa shirika la Haki Zetu Tanzania Gervas Evodius,amesema ukatili wa kimtandao ni miongoni mwa ukatili ambao wanafanyiwa watu wengi na una madhara makubwa.
Ambapo ukatili wa kimtandao unaumuathiri mtu kisaikolojia na kusababisha hata kujiua,kumharibia mtu malengo yake mfano unakuta binti mdogo picha zake za utupu zimesambaa katika mitandao hali hiyo inaweza kusababisha kujifungia katika kupata fursa mbalimbali ambapo hatoweza kuajirika kwenye taasisi au ajira nyingine.
Pia baadae atahitaji kuwa mzazi kama mama watoto wake watakua wataona kwa sababu kitu kikiwekwa kwenye mtandao maana yake kitaendelea kuwepo kwa muda mrefu.
Amesema,suala la ukatili wa kimtandao lina wigo mpana zamani aliona kuwa baadae itakuja kuwa changamoto kubwa kwa sababu jamii ilipokea teknolojia bila ya kuwa imejipanga.
“Tulishindwa kuchambua sisi kama taifa tunataka vitu gani haswa ambavyo kwetu vitakuwa ni vya muhimu kwenye mitandao,ukiangalia sasa hivi kwenye mambo ya utanda wazi kuna vitu ambavyo watu wanaiga kwenye mataifa mengine,wanaona labda ndio mtindo wa maisha hivyo wanaamua kuishi katika mtiririko huo huo,”amesema Gervas.
Pia amesema,watu wenye ushawishi mkubwa kwenye jamii wamechangia sana kuwepo kwa mmomonyoko huo wa maadili ya kimtandao kwani kuna watu wanataka kuwa maarufu kwa sababu amemuona fulani amekuwa maarufu,hivyo yupo radhi afanye kitu chochote ili awe maarufu.
“Watu maarufu kama wamefanya halafu watu wakaona hajachukuliwa hatua kali,jamii inaona kama kitu cha kawaida basi na mwingine anafanya,hata ukiangalia maoni(comments) ya watu kuwa ukitaka kuwa maarufu achia video yako unakuwa maarufu,watu wengine wapo tayari kufanya chochote ili wawe maarufu,”amesema Gervas na kuongeza
“Wakati mwingine watu wanataka wapate ela,wanawarubuni watu wanaiga hizo video na wanasambaza kwenye mitandao,kwa lengo la kupata ela au umaarufu,”.
Gervas amesema, changamoto ya kusambazwa kwa video zilizo kinyume na maadili katika mitandao ni kuwa jamii haikuwafundisha mabinti na vijana jinsi gani ya kutumia mitandao ya kijamii baada ya teknolojia kukua iliwaacha tu wafanye vyote.
Aidha haikuwafundisha vitu gani ambavyo anapaswa ajirekodi video au kitu gani asichukue video,hivyo ikasababisha wao kuona kuwa kila kitu wanaweza kuchukua video hali inayosababisha kuwa rahisi kuweza kurubuniwa na kuweza kusambazwa.
Hivyo elimu ya matumizi ya mtandao bado ni changamoto,wadau na serikali kwa pamoja wanahitajika kutoa elimu na kuangalia ni kitu gani au maudhui gani yanayoenda kwenye mtandao vinginevyo hivyo vitu vitaendelea kuwepo.
“Lakini tunatakiwa tuchambue maudhui ambayo yapo mitandao,tutatambua sisi kwa jamii yetu tunataka maudhui gani,kwani video hizo za utupu zinaweza kuwa nzuri katika nchi nyingine na zisiwe nzuri kwetu ingawa serikali yetu imejitahidi kuzifunga site ( mitandao yenye maudhui ya ngono) lakini ni wakati tumeisha chelewa watu wameisha kuwa wazi(exposed) na hivyo vitu na wanaendelea kusambaza kwa njia zingine,” amesema Gervas.
Hata hivyo amesema,sheria pekee yake haijawai kufanya kazi ikafanikiwa kwani sheria inaweza kuwepo ndio maana leo unaambiwa ukifanya hivi ni dhambi lakini bado watu wanafanya mfano kuiba ni kosa lakini watu wanaendelea kuiba,kwaio sheria pekee yake haijawai kuwa mwarobaini wa tatizo lolote katika jamii.
Amesema, jambo linaloweza kuwa mwarobaini wa kudumu inawezekana ikawa ni elimu,maana watu wakibadilika katika mtazamo,wakijua madhara yake hata kama sheria haitakuwepo hawata fanya kitendo hicho kwa sababu tayari ana uelewa.
“Maana unaona sheria inaweza kuwepo na vitendo vikawepo sasa tuendelee kutoa elimu na tuwaoneshe madhara ya ya picha au video zisizo na maadili hasa kwa watoto waliopo shuleni na vijana ambao bado wapo vyuoni kwa sababu watoto wadogo ni rahisi kuonewa ambao bado wako shuleni au mtaani ni rahisi kurubuniwa wakiwa katika mapenzi akiambiwa nitumie video zako na yeye akatuma tu,”amesema Gervas.
Vilevile amesema,wanatakiwa kufundisha kuwa hawapaswi kumuamini mtu yoyote maana mara nyingi wanaowafanyia ukatili ni wale watu ambao wanawaamini na kutuma hizo video.
Maana wanawatumia wale ambao wanawaamini ambao ndio wanaosambaza hizo video,hivyo wafundishwe kuto muamini mtu yoyote kwani anaweza kuwa na nia ovu dhidi yao,pia wafundishwe kuwa hata wakihifadhi video hizo kwenye laptop,simu,CD vinaweza kupotea na watu wasio wema wakaviokota na kuzisambaza.
“Kwaio tuwafundishe sababu sheria ipo lakini mtu ataiba simu yangu atasambaza kama kuna video hizo sheria itaniadhibu mimi lakini aliyesambaza ni mtu mwingine hivyo tuwaambie wasipige hizo video wala picha ndio itakuwa mwarobaini wa tatizo hilo kwani sheria pekee haiwezi kumaliza changamoto hiyo,”amesema Gervas.
Sanjari na hayo amesema,familia ikae na kuchunguza mienendo ya watoto wao, waangalie vitu gani wanaposti kwenye mitandao,vitu gani wanaangalia kwenye runinga nyumbani na kwenye mitandao kuanzia watoto wadogo maana akiwa mkubwa au akifikia umri fulani anakuwa tayari ameathirika na tabia hizo na asikilizi kitu chochote na anaona watu wanaishi hivyo ni muhimu kama wazazi kuongea na watoto ili kuepuka vitu kama hivyo.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Christiana Mwambola, amesema vitendo vya ukatili wa kimtandao siyo kitu kizuri,sababu ukiangalia mila na desturi zetu haziruhusu vitu kama hivyo kuonekana peupe.
Sababu ya utanda wazi kumekuwa na simu hata watoto wadogo ambao ni wanafunzi wanamiliki simu,kwa sababu ya mtandao wanatumiana picha za utupu tofauti na zamani walikuwa wanaandikiana barua.
Mwambola amesema, ingawa sheria hairuhusu mtoto mdogo kumiliki simu,lakini unakuta kuna baadhi ya wazazi wanawapa watoto simu sasa tunaona mitandao inavyoathiri watoto na watu wazima pia.
“Lengo la mtandao ni mawasiliano,lakini jinsi inavyotumika kwa jamii zetu ni vibaya hasa kwa watu wazima na watoto kila mtu anatumia tofauti hali inayoongeza ukatili sana mtaani kwa sababu watu wanapata uelewa wa namna ya kufanya vitendo vya ukatili,kwa watu wengine,”amesema Mwambola.
Amesema sheria zikisimamiwa kwa umakini na kwa vitendo mfano ya mtoto na suala la kutuma picha za utupu kati ya mtu na mtu kwa maana ya mke na mme au mme na mke lisiruhusiwe inaweza kusaidia kumaliza ukatili wa kimtandao.
Naye Ofisa Dawati la Jinsia na Watoto Sekou-Toure (one stop center) Gift Msowoya, amesema wanapokea kesi za ukatili wa kimtandao masalani wanaofanyiwa ni watu wote watoto na watu wazima.
Ambapo akija na uthibutusho kwamba amarekodiwa,wanachukua maelezo ya yule mlengwa,wanampa ushauri nasaha kisha wakimaliza kumuhoji wanamushauri namna ya kufungua kesi.
Kwani kuna wengine wanaogopa kuwa wakifungua kesi inaweza kusambaa zaidi,lakini tunamueleza kuwa watalifikisha mbele ya sheria na litabakia mikononi mwa sheria huku wakichukua hatua ya kudhibiti kwa kuwachukulia hatua wale watu ambao wamefanya hivyo ili video isiendelee kusambaa sehemu yoyote ile.
Pia amesema,wamekuwa sehemu ya kuwapa watu elimu kwani siyo wote wanaorekodiwa wanakuwa wanajua madhara ya vitu hivyo,kuna anarekodiwa anajua kuwa yupo kwenye starehe lakini hajui kwamba mbele wanaweza kugombana hivyo mtu akaamua kusambaza.
“Tunaendelea kuwapa elimu watu wote siyo wahanga pekee hata ambao hawajatendewa vitendo hivyo ili wasijiingize kwenye kundi au vitendo vya kuchukuliwa video za utupu na kisha kusambazwa kwenye mitandao, uzuri sheria zipo wazi ,tunaendelea kuelimisha watu ili wajue imetungiwa sheria maalum ya matumizi mabaya ya mtandao na wanapokuja tunawasaidia,”amesema Msowoya.
More Stories
SACP Katabazi Elimu ya usafirishaji wa kemikali muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume