Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
IMEELEZWA kuwa ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na jinsia ni miongoni mwa sababu inayopelekea wanafunzi wa kike kupata mimba katika umri mdogo pamoja na ndoa za utotoni sanjari na kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Kwa kutambua changamoto hiyo shirika la Wadada Solution on Gender Based Violence,wamejikita katika utoaji wa elimu hiyo kwa kata mbili za Kitangiri na Pasiansi ambazo ni miongoni mwa maeneo ambayo jamii yake ina wanafunzi ambao wanakosa elimu ya afya ya uzazi na jinsia kupitia mradi wa Haki ya Binti.
Hayo yameelezwa na Ofisa Mradi wa mradi wa Haki ya Binti awamu ya pili kutoka shirika la Wadada Solution on Gender Based Violence,Elihaika Mugenyi, mara baada ya kumalizika kwa semina ilio wakutanisha maofisa ustawi,Polisi,wahudumu wa afya na watendaji Kata ilioandaliwa na shirika hilo.
Yenye lengo la kuwajengea uwezo wadau hao ili kujua namna gani wanaweza kusaidia jamii katika kutoa taarifa sahihi dhidi ya vitendo vya ukatili.
Mugenyi amesema, utafiti uliowai kufanyika hapo awali ulionesha kwamba Kata ya Kitangiri na Pasiansi ina jamii ya wanafunzi wengi wanaokosa elimu ya afya ya uzazi na jinsia,ambayo ina changia wao kupata mimba,katika umri mdogo na wengine kuolewa katika umri mdogo.
Hivyo kutokana na changamoto hiyo shirika liliona lina nafasi kubwa katika kutoa mchango wa elimu katika kata hizo,ili kupunguza idadi ya wanafunzi ambao wanapata mimba na kuolewa katika umri mdogo sanjari na vitendo vya ukatili.
Amesema,wanatekeleza mradi wa miaka 3 wa Haki ya Binti awamu ya pili,katika Wilaya ya Ilemela kwa Kata za Kitangiri na Pasiansi huku lengo likiwa ni kuwajengea uwezo vijana wa namna gani wanaweza kupinga mimba katika umri mdogo,kuepukana na ndoa za utotoni lakini pia na masuala yote ya ukatili.
Pia amesema,wanaendelea kuongeza uelewa kwenye jamii ili kuhakikisha kwamba miaka ijayo hakuta kuwa na jamii ambayo ina shughulika na masuala ya ukatili kwa watoto na wanawake.
Mbali na hayo amesema, changamoto nyingine wanaona jamii hizo wazazi bado wanashikilia mila na desturi ambazo zinakuwa zinakosesha mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kusoma,haki ya kufanya maamuzi binafsi kwa sababu mila zinamlazimisha kuolewa akiwa katika umri mdogo.
“Tunatamani kuona kwamba tunapata wanawake ambao watakuwa ni viongozi wazuri wa baadae,wanaoweza kusimama na kutetea mambo yao ya msingi,awamu ya kwanza ya mradi tunaweza kusema kwamba matokeo ni makubwa tumeweza kukuza uelewa katika jamii,ya Kitangiri na Pasiansi pia ushirikiano mzuri,”amesema Mugenyi.
Kwa upande wake Ofisa Dawati la Jinsia na Watoto Sekou- Toure(One stop center) Gift Msowoya, amesema hali ya ukatili siyo nzuri sana hususani kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18, hasa katika ukatili wa kingono.
“Tunapopata taarifa tunajua kwamba watu wanaelimika,hapo tunaweza kusema ni nzuri maana kama umekaa ofisini halafu hupati taarifa unajua kuna shida japo kuwa hali ni mbaya lakini kuna uzuri wake kwamba elimu inafika watu wanajua umuhimu wa kuripoti haya matukio na madhara yake katika jamii na anaenda kutoa taarifa katika sehemu husika,” amesema Gift.
Daktari wa kituo cha afya Pasiansi Dkt. Mirian Elias,amesema madhara yanayoweza kutokana na vitendo vya ukatili ni pamoja na kuathirika kisaikolojia kutokana na aina ya ukatili ambao amefanyiwa.
Pia amesema,kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto yamesaidia elimu iwepo katika jamii,shule na kwenye vyuo ya kujua nini maana ya ukatili, wapi aende kutoa taarifa ili aweze kupata msaada.
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika