Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Seriali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imedhihirisha dhamira ya kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya kazi katika sehemu za kazi kwa lengo la kuimarisha mahusiano mema na kuongeza ufanisi wa kazi na mashauriano kati ya waajiri na wafanyakazi.
Hayo ameeleza Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Prof. Jamal Katundu wakati wa ufunguzi wa kikao cha Mashauriano na Wadau wa sekta ya habari kilichofanyika ukumbi wa mikutano uliopo jengo la PSSSF Jijini Dodoma, Februari 16, 2022.
Alieleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Kazi ina jukumu la kufanya kaguzi katika sehemu za kazi, kutoa elimu, kuratibu utoaji wa Vibali vya Ajira kwa raia wa kigeni pamoja na kusimamia shughuli za uwakala wa Huduma binafsi za Ajira hapa nchini.
“Katika kuendelea kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa sheria za kazi nchini, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali na kufanya marekebisho ya sheria za kazi kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa wananchi hivyo leo kikao hiki kitatoa fursa kwenu kujulishwa kuhusu sekta hii ya kazi” alisema Prof. Katundu
Aliongeza kuwa, Sekta ya habari ni muhimu sana katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo kutokana na mchango huo wanahabari na wafanyakazi wengine wa sekta hiyo, serikali inawajibu wa kusimamia hayo ili wafanyakazi waweze kupata haki zao kwa mujibu wa sheria za kazi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni sikivu na imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi hapa nchini ili kupunguza migogoro ya kazi,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu alitoa rai kwa waajiri, wafanyakazi na Vyama vya Wafanyakazi kushirikiana katika kuzingatia misingi ya kuimarisha mahusiano mema sehemu za kazi.
Kwa upande wake Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Suzana Mkangwa alisema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali katika kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa sheria hizo, ikiwemo kutowapatia wafanyakazi Mikataba ya Ajira, kutowapa haki wafanyakazi kujiunga na vyama vya Wafanyakazi, kutowasajili na kuwachangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kuwaachisha kazi wafanyakazi bila kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria pamoja na madai ya mishahara na stahiki nyingine.
“Idara ya Kazi kushirikiana na Wizara ya Habari tumeona umuhimu tuwe na kikao cha mashauriano na wadau wa sekta hii ili kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuimarisha mahusiano mema katika maeneo ya kazi,” alisema Kamishna Mkangwa
Pia, alisema kuwa Idara ya Kazi itaendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusu kuhakikisha inawatumikia wananchi ipasavyo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (Maelezo), Rodney Mbuya alisema kuwa Sekta ya habari ni sekta nyeti na ina mchango mkubwa sana katika ustawi wa Taifa, hivyo alisisitiza uwepo wa maelewano mazuri baina ya wadau katika sekta hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi Watafiti, Wanataaluma na Washiriki wake (RAAWU), Jane Mihanji alisema kuwa kikao hicho kimekuwa na tija kwa wadau wa sekta hiyo ya habari, hivyo alihimiza wafanyakazi katika sekta hiyo kuhakikisha wanakuwa wanajiunga kwenye vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi ili kuwa na mikakati ya pamoja ya kuendeleza sekta hiyo.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania