Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Uhifadhi mazingira na wanyamapori ndio urithi wa vizazi vijavyo ambao ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya utalii nchini na maendeleo ya taifa.
Kwa kilitambua hilo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kupitia kitengo cha Malihai Clubs of Tanzania Kanda ya Ziwa,wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu na faida za uhifadhi wa wanyamapori.
Akizungumza na majira/ timesmajira Mhifadhi wa Wanyamapori TAWA kitengo cha Malihai Kanda ya Ziwa Omary Mhando, amesema wanaelimisha wanavijiji watambue umuhimu wa uhifadhi na faida wanazozipata wananchi kutokana na uhifadhi wa wanyamapori.
Mhando amesema,pia wamekuwa wakitembelea shuleni na kuwaelimisha watoto(wanafunzi) ili wajue umuhimu wa uhifadhi wakiwa wadogo na watakapokuwa wawe wahifadhi bora.
“Katika shule huwa tunawafundisha watoto wajifunze mapema umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti ndio maana tunagawa miche ya miti bure shuleni,” amesema Mhando.
Amesema,zipo faida za uhifadhi wanyamapori nchini ikiwemo upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na utalii,uboreshaji wa miundombinu na huduma za jamii,kutoa ajira za kudumu na za muda.
Kuimarika na kuendeleza utamaduni wa makabila mbalimbali,jamii kupata chakula pamoja na kuimarika kwa uhifadhi wa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.
Pia amesema mbali na elimu ya uhifadhi pia wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi juu ya wanyamapori 7 ambao ni hatari na waharibifu na namna ya kujihami nao.
Wanyamapori hao ambao wanajulikana kwa mujibu wa Sheria ya uhifadhi Namba 5 ya mwaka 2009 ni tembo, simba,nyati, fisi, kiboko,faru na mamba.
“Madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hatari na waharibifu ni kama uharibifu wa mazao shambani,vifo vya mifugo,majeraha kwa watu,vifo kwa watu hofi kwa jamii pamoja na kuambukizwa magonjwa kwa watu na mifugo,” amesema Mhando.
Sanjari na hayo amesema,elimu ya uhifadhi wanatoa kwa jamii vijijini mwambao mwa mapori ya akiba ikiwemo Maswa, kijereshi na ikolongo Grumet ambapo jamii inayozunguuka mapori hayo imekuwa ikielimishwa juu ya athari za kuingiza mifugo hifadhini , wanyamapori hatari na waharibifu,malipo ya kifuta jasho/ machozi,uhifadhi wa wanyamapori kwa utalii na uendelevu,nyara za serikali ,sheria ya uhifadhi na sera vijijini.
Hata hivyo amesema ikielimishwa jamii juu ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira inasaidia kuondoa migogoro baina ya wahifadhi na wananchi.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda