Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Afya ,Ummy Mwalimu amewaasa watanzania kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan saratani kwa kuzingatia mlo kamili nakufanya mazoezi na Kuzingatia ulaji wa matunda na mboga mboga za kutosha, kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kuepuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kuepuka ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi.
Ummy amesema hayo ikiwa leo ni siku ya saratani Dunia huku Tanzania ikikadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani 42,060 kwa mwaka huku takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Amesema kutokana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zinaonesha kuwa tatizo la saratani nchini Tanzania limekuwa likiongezeka siku hadi siku ambapo inakadiriwa kuwa katika kila watu 100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani.
Ummy ameeleza hayo Jijini hapa leo wakati akiongea na wananchi katika kituo cha afya Makole ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Saratani Duniani yaliyolenga kutoa elimu ya kinga na kuelimisha wananchi na hatua za kuchukua kukabiliana na ugonjwa huo.
Ameeleza kuwa takwimu kutoka kwenye kanzi data zilizoanzishwa kwa Kanda , zinaonesha kwamba wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa.
Aidha, ameeleza kuwa taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliyopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume (21%), Saratani ya Koo (11.8%),Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%).
Pia ametaja aina ya Saratani inayoongoza kuwaathiri wanawake ni Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8) huku akisema kuwa ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora.
“Kuna mtindo mbaya wa maisha unaochangia saratani kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi,”amesema.
Ameeleza zaidi kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.
Amesema kwa kutambua hilo, Serikali imeongeza juhudi za kuhakikisha kuwa uelewa katika jamii kuhusiana na tatizo hili unaongezeka kwa kuandaa mtaala wa mafunzo mashuleni unaozungumzia magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kudhibiti na kuanzisha Program ya taifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Akieleza takwimu za Dunia,Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Atomic Research on Cancer-IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani sawa na asilimia 50.
Hivyo amesisitiza kila mmoja kupima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya na kwamba endapo atatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani utashauriwa kutumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya.
“Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani ,na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha,”amesisitiza.
Siku ya Saratani Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Februari ambapo ilianza kuadhimishwa mwaka 2000 mjini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa Dunia wa saratani ,Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani kwa mwaka 2022 ni Huduma za saratani sawa kwa wote.’
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu