Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) amezindua rasmi Mafunzo kwa Watoa Huduma za Utalii nchini kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Bustani jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Masanja amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii kuhusu namna ya kukabiliana na UVIKO 19.
“Mafunzo haya yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii nchini juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama pamoja na kuboresha huduma wanazotoa na hatimaye kimarisha ushindani wa nchi katika masoko mbalimbali ikiwemo kuvutia watalii wa kimataifa kuja nchini hasa katika kipindi hiki cha mtazamo mpya wa utoaji huduma za utalii na usafiri kukabiliana na UVIKO-19 yaani ” the new normal of tourism and travel ” amesisitiza Mhe.Masanja.
Amemshukuru Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambao utekelezaji wake umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwafikia takriban watoa huduma 3,900 katika sekta ya utalii katika mikoa 26 nchini Tanzania.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Philiph Chitaunga amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuendelea kujengea imani watalii na ulimwengu kwa ujumla kuwa Tanzania imedhamiria kupambana na janga la UVIKO 19.Pia, amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama.
Mafunzo hayo yamehusisha watoa huduma mbalimbali katika tasnia ya ukarimu na huduma za malazi na chakula kama vile katika hoteli, loji na kambi za kitalii; aina mbalimbali za waongoza watalii; watoa huduma katika shughuli za utalii wa kupanda mlima, uwindaji wa kitalii na utalii wa utamaduni; wakala wa safari za kitalii; wakala wa usafiri wa anga; na wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika na kutoa huduma.
More Stories
Walengwa TASAF Korogwe TC watakiwa kuchangamkia fursa
Rais Mwinyi aipongeza NMB
Wananchi wa Ikuvilo watakiwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao