November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shirika la CIAT,TALIRI wakamilisha utafiti wa malisho ya mifugo

Na Omary Mtamike,TimesMajira Online, Mbeya

TAASISI ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Utafiti la (CIAT) wamewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa uliotekelezwa kwa miaka 4 katika kanda ya nyanda za juu kusini.

Mgeni rasmi katika kikao cha kuwasilisha taarifa hiyo  kilichofanyika kwenye Ukumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vincent Anney amezipongeza pande zote kwa hatua hiyo ambapo ametoa rai kwa watekelezaji wa matokeo ya utafiti huo kuhakikisha elimu na ujuzi uliopo kwenye taarifa hiyo unaenea kwa wafugaji wote nchini.

Mfugaji kutoka kitongoji cha Itebe Wilayani Rungwe, Ezekia Kimanga (kulia) akitoa  zawadi kwa niaba ya wafugaji wote wa Wilaya ya Rungwe kwa Afisa Utafiti wa Shirika la kimataifa la utafiti la CIAT aliyekuwa akifanya kazi kwa upande wa Nyanda za juu kusini, Beatus Nzogela ikiwa ni ishara ya kutambua mchango uliotolewa na Shirika hilo kwa wafugaji wa kanda hiyo kwa kipindi cha miaka 4 ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa uzalishaji malisho ya mifugo  yaliyoboreshwa ambao jana ndio umefikia tamati.

“Ili tuwe na ufugaji wenye tija ni lazima utafiti unaombatana na majaribio ufanyike kama ambavyo mradi huu umefanya kwa kushirikiana na Serikali hivyo nashauri iundwe kamati maalum ya kufuatilia uendelezaji wa yote yaliyofanyika wakati wa mradi ili tutumie fursa tuliyoipata kusonga mbele badala ya kusubiri mradi mwingine” Amesema Dkt. Anney.

Dkt. Anney amebainisha kuwa mradi huo umewahamasisha wafugaji kuzalisha malisho ambayo yameleta tija na kuongeza  uzalishaji wa  mazao yanayotokana na mifugo  hivyo ametoa rai kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mipango madhubuti ya kutafuta masoko ya mazao hayo.

“ Uzalishaji mkubwa wa malisho yaliyoboreshwa unaofanywa na wafugaji wetu hivi sasa kupitia mradi huu umesababisha uzalishaji wa maziwa mengi hivyo wafugaji wameanza  kukosa soko la maziwa hayo na kwa sababu hawatumii nguvu kubwa kwenye kuyazalisha tofauti na ilivyokuwa awali wanaweza kuona hiyo hali ni ya kawaida kwa hiyo  ni lazima tuwasaidie ili maziwa hayo yawaletee tija ya kutosha” amesisitiza Dkt. Anney.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba mbali na kuonesha furaha ya kuhitimisha mradi huo kwa mafanikio  ameweka wazi  kuwa Taasisi yake ipo tayari kushirikiana na wadau wote wenye lengo la kuendeleza sekta ya mifugo nchini kama ilivyofanya na Shirika hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dkt. Vincent Anney (kulia) akieleza namna anavyovutiwa na shughuli za ufugaji muda mfupi baada ya kuwasili nje ya Ukumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya jana. Wengine pichani kutoka kulia ni Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt. Jonas Kizima, Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT, Dkt. An Notenbaert, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba, Kaimu Meneja wa TALIRI-Uyole Dkt. Edwin Chang’a na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Dkt. Angelo Mwilawa.

“Mbali na utafiti wa malisho, Taasisi yetu pia inafanya utafiti katika vyakula vya mifugo na ulishaje wake, Uzalishaji, uzazi, afya ya mifugo na haki za wanyama ambapo ili kutekeleza shughuli zake Taasisi yetu inapata fedha kutoka Serikalini, vyanzo vyetu vya ndani na kupitia wadau wa maendeleo kama CIAT na wengineo” Ameongeza Prof. Komba.

Prof. Komba amesema kuwa hivi sasa Taasisi yake inaendelea na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti mpya unaolenga kutengeneza teknolojia na mtandao wa ushauri katika ubora wa maziwa ambao unafanyika katika kanda ya Mashariki ya Taasisi hiyo iliyopo mkoani Tanga, utafiti wa vyakula vya mifugo vinavyojumuisha michanganyiko ya bei rahisi  inayompa mnyama afya bora.

“Lakini pia tuna  majaribio mengi sana huko vituoni yanayohusu  uzalishaji  mifugo, matunzo ya mifugo, unenepeshaji, uchambuzi na kutathmini mifugo na mawe lishe katika eneo la ulaji na ukuaji wa mbuzi zoezi linaloendelea kwenye kituo chetu cha Kongwa” Amesema Prof. Komba.

Naye Mwakilishi wa Shirika la CIAT, Dkt. An Notenbaert ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano waliouonesha wakati wote wa kutekeleza mradi huo ambao pia ulilenga kufanya utafiti wa malisho bora kwa mifugo na kuandaa taarifa ya utafiti itakayotumiwa na watekelezaji wa Sera katika kuinua sekta ya mifugo nchini.

“Pia nitoe shukrani zangu kwa Shirika la IFARD kwa kukubali kutoa fedha za kutekeleza mradi huu hivyo iwaombe wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo nchini pamoja na mradi huu kufikia kikomo, waendelee kusambaza mbegu za malisho haya yaliyoboreshwa katika maeneo mengine yaliyosalia hapa nchini ili kila mfugaji anufaike na malisho haya” Amesema Dkt. Notenbaert.

Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT, Dkt. An Notenbaert (katikati) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vincent Anney (kulia) kalenda ya Shirika hilo ya mwaka 2022 muda mfupi baada ya Dkt. Vincent kufunga kikao cha uwasilishaji wa  taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa kilichofanyika jana kwenye kumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa.

Kwa upande wa mmoja wa wafugaji walionufaika kutokana na mradi huo kutoka mkoani Njombe, Juliana Mlagala amesema kuwa malisho hayo yaliyoboreshwa yamewaongezea ari ya kuendelea kufuga baada ya kuonesha matokeo chanya kwenye mifugo yao.

“Tangu tuanze kutumia malisho haya yaliyoboreshwa tumekuwa na uhakika wa chakula bora cha  mifugo yetu na tumeokoa muda mwingi sana ambao zamani tulikuwa tunaupoteza kwenda kutafuta malisho ya mifugo yetu  hivyo ninaomba Serikali iendelee kutuletea miradi ya aina hii ili tuendelee kunufaika kutokana na shughuli hizi za ufugaji” Amesema Mlagala.

Mradi wa Utafiti wa kilimo cha  malisho yaliyoboreshwa bila kuathiri mazingira umetekelezwa na Shirika  la kimataifa la Utafiti la CIAT kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Idara ya Mafunzo, Utafiti na Ugani kupitia taasisi yake ya TALIRI ambapo umetekelezwa kwa miaka 4 katika Halmashauri 3 ambazo ni Mufindi, Njombe na Rungwe.