November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MISA TAN yawapiga msasa Waandishi Dodoma kuhusu sheria za habari

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

TAASISI ya Vyombo Vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara tawi la Tanzania (MISA TANZANIA) mwishoni mwa wiki imewajengea uwezo waandishi wa habari mkoa wa Dodoma kuhusu sheria mbalimbali za habari.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa MISA TAN,afisa Habari wa taasisi hiyo Jackline Jones ambaye pia ni mratibu wa mradi huo wa kuwajengea uwezo unaofadhiliwa na taasisi ya International Media Support(IMS) amesema lengo kuu la semina hiyo ni kuwajengea uwezo waandishi hao ili kutambua maudhui ya sheria hizo.

“Tunachofanya kupitia semina ni kuwaonesha na kuwasaidia Waandishi wapate Uelewa wa sheria ambazo zinasimamia tasnia yao.”Amebainisha  Jackline

Afisa huyo amesema kupitia semina hiyo waandishi watakuwa na uwezo wa kushiriki mijadala mbalimbali ikiwemo ile ya mabadiliko ya baadhi yaa vifungu katika sheria hizo ambazo zinaonekana kuminya uhuru wa kujieleza.

Kwa upande wake mwezeshaji wa semina hiyo Jesse Mwandishi na Mhariri Mwandamizi Jesse Kwayu  amebainisha kwamba yapo mambo mengi mazuri kwenye sheria za habari  lakini mazuri hayo yanafunikwa na vifungu vichache vinavyominya uhuru wa habari na kujieleza.

Kwayu pia amewataka waandishi wa habari kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili wawe na uelewa juu ya vifungu mbalimbali katika sheria hizo.

“Sheria tulizonazo ukizisoma kwa wepesi utaziona ni nyepesi lakini ni sheria nzito sana,na Mwandishi ili akamilike lazima azifahamu sheria hizi”-amesema Kwayu

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia mkoa wa Dodoma Menas Muhumpa amewataka waandishi wa Habari kushirikisha taasisi hizo katika mapambano ya kudai haki kujieleza kwa vile ni matakwa ya katiba.
Muhumpa amesema haki hiyo inamgusa kila mwananchi hivyo ni vyema taasisi zote zikaungana kupigania haki hiyo.

“Msione hili jambo ni kwenu peke yenu,kama hivi MISA TAN walivyotushirikisha basi iwe fursa kwa taasisi nyingine za habari kuona umuhimu wa kushirikisha taasisi za kiraia ili kuunganisha nguvu na kuwa sauti ya pamoja.” Amebainisha Muhumpa.


“ Tuungane pamoja katika harakati za kudai uhuru wa habari,linapomtokea mwenzako leo kesho linaweza kuwa kwako.Mmoja wetu akipatwa na tatizo tusimuache yeye na chombo chake tu.” Ameelezea Munuo.

Kwa upande wa baadhi ya Wandishi washiriki wa mafunzo hayo,wamewataka waandishi wote kuungana pamoja katika kutetea maslahi ya tasnia.
Merciful Munuo ni mmoja wa Wanahabari walioshiriki semina hiyo amesema kuna mambo mengi yanayosonga utendaji wa wanahabari nchini lakini kwa mara kadhaa waandishi hawatoi ushirikino katikakutatua changamoto za wengine.