Na David John
WADAU wanaofanya biashara ya betri chakavu nchini, wameshauriwa kutumia vifaa vya kujikinga wakati wa kukusanya na kuuza bidhaa hizo, ili kulinda afya za wananchi na kutunza mazingira.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chilambo General, Gideon Chilambo wakati akitoa elimu kuhusu ukusanyaji na umwagaji wa maji ya betri kwenye warsha iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Pure Earth Tanzania.
Chilambo alisema kuna ombwe kubwa la elimu kuhusu namna ya ukusanyaji, umwagaji maji, utunzaji na usafirishaji wa betri chakavu hali ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.
Alisema wanunuzi wengi wa betri chakavu wamekuwa wakimwaga maji ya betri ambayo yana tindikali bila kufuata sheria na taratibu hali ambayo ni hatari kwa maisha yao.
“Mimi nimetoka huko kwenye ununuzi wa betri na kumwaga maji bila kufuata taratibu, baada ya kupata elimu sasa nafuata taratibu zote za kiafya na usalama wa mazingira, hivyo nawaomba na nyie mbadilike ili kulinda afya za wananchi na mazingira,” alisema.
Chilambo alisema ili kuwa salama wakati wa kukusanya, kumwaga tindikali, kuhifadhi na kusafirisha betri unapaswa kuwa viatu vya buti, kofia, miwani, nguo maalum, glove na vifaa vingine ambavyo vitalinda mwili usidhurike.
Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wanunuzi na waauzaji wa betri chakavu kuchimba mashimo ambayo yamewekwa zege na sakafu ili kuhifadhia maji hayo na baadae kuwaita wataalam ili kuyaharibu yasiwe na madhara na wanadamu.
“Nitumie nafasi hii kuliomba Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kutoa elimu kwa wakusanyaji wa betri wasio rasmi kwani wanahatarisha afya zao, wananchi na mazingira hasa kwa kitendo cha kumwaga tindikali chini,” alisema.
Aidha, Chilambo amewataka wafanyabishara hao wadogo kuanza maandalizi ya kusajili kampuni zao ili wawe rasmi hali ambayo itawezesha kupata zabuni mbalimbali zinazotangazwa na makampuni yanayouuza betri chakavu.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk. Daniel Sabai alisema iwapo kutakuwa na Sera ambayo imejikita kwenye madini ya risasi ni wazi mazingira na afya za wananchi zitakuwa salama.
Alisema tafiti zinaonesha madini hayo yanasababisha magonjwa ya figo, udumavu, uwezo wa akili na uharibifu wa mazingira hali ambayo ikiachwa itaweza kuleta athari zaidi.
Mratibu wa Pure Earth Tanzania, Abdallah Mkindi alisema wameweza kupata hali halisi kupitia warsha tatu ambazo wameandaa jambo ambalo litawasaidia kuishawishi Serikali katika kukabiliana na biashara hiyo ya betri chakavu kisera na kisheria.
Alisema Pure Earth, kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), wamedhamiria kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa salama ndio maana wameamua kushirikisha makundi yote ambayo yanajihusisha na biashara hiyo.
“Tumeamua kukutana na makundi yote yaani kuanzia wasimamizi wa sheria na sera, wafanya biasharam, wachakataji na wanaohifadhi lengo ni kuwa kitu kimoja katika kudai sera na sheria mpya mahususi ya berti betri chakavu na ukweli umeonekana kuwa bado kuna ombwe la elimu,” alisema.
Amesema Tanzania ina sheria ya mazingira ambayo inazungumzia taka hatarishi kwa ujumla, lakini sheria inayozungumzia taka hatarishi za betri chakavu haipo jambo ambalo limewasukuma kuanda mapendekezo ya sera na mkakati.
Amesema kutokana na maelezo ya washiriki ni wazi kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kuweza kutambua maeneo ambayo yameharibika yamechafuliwa kutokana na umwagaji wa tindikali unaofanywa na wanunuzi wa betri chakavu.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM