November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari watakiwa kuandika habari sahihi kuhusu UVIKO-19

Judith Ferdinand, Mwanza

Waandishi wa habari nchini,wametakiwa kuandika habari sahihi kuhusu UVIKO-19,ili wananchi wapate taarifa zitakazo wasaidia kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwani katika kipindi hiki upatikanaji wa taarifa ni sehemu muhimu kwa mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Hayo yamesemwa na Mtaalamu wa Mawasiliano Rose Haji Mwalimu wakati akiwasilisha mada katika warsha ya kimtandao ya waandishi wa habari wanawake iliokuwa na mada juu ya vyombo vya habari na dhana ya chanjo ya UVIKO-19 kwa wanawake.

Warsha hiyo ilioandaliwa na Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari Wanawake wa Redio na Televisheni(IAWRT) Tanzania.

Mwalimu amesema, waandishi wa habari wanatakiwa kutoandika habari za kutisha zinazoweza kusababisha hofu huku wakitakiwa kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu.

Amesema,katika dharura za afya ya umma kama vile janga la UVIKO-19,linaloendelea hatua moja muhimu ya kuokoa maisha ni mawasiliano ya kuondoa hatari.

Ili kufanya hivyo kwa ufanisi,wawasilishaji wa habari hatari wanahitaji uelewa mzuri wa mitazamo ya washikadau,wasiwasi,imani, ujuzi pamoja na desturi zao.

Pia amesema, wawasilishaji lazima watambue mapema na kudhibiti uvumi,habari potofu na changamoto zingine za mawasiliano.

“Hii ni kwa sababu watu wana haki ya kujua jinsi ya kulinda afya zao na kuwa na wajibu wa kuchukua maamuzi sahihi ili kujilinda wao wenyewe,wapendwa wao na wake walio karibu nao,”amesema Mwalimu.

Kwa upande wake mmoja wa waandishi walioshiriki warsha hiyo Neema Emmanuel wakati akizungumza na majura mara baada ya kumalizia kwa warsha hiyo,amesema ameweza kupata elimu ambayo itamsaidia katika kazi zake za kuhabarisha umma hususani kipindi hiki ambacho dunia na taifa lipo katika mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Pia amesema,kama waandishi wanajukumu kubwa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya UVIKO-19,kwa kuhakikisha wanahabarisha jamii taarifa zilizo sahihi kutoka kwa wataalamu.