Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa amewataka Wanaume kujitokeza kwa wingi kupima Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ili kujua afya zao badala ya kukaa na kutegemea majibu ya wake zao.
Mh.Majaliwa amesema hayo leo wakati akifungua Kongamano la kisayansi katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani lililofanyika katika Ukumbi wa Mbeya Modern Hoteli iliyopo jijini Mbeya.
Aidha amesema kuwa .mwaka 2018 kulifanyika utafiti ambao ulibainisha kuwa wanaume wengi wanakwepa kwenda kupima maambukizi ya Ukimwi na badala yake wanategemea majibu ya wake zao baada ya kupima pindi wanapoenda kujifungua.
Amesema ili malengo ya Serikali ya ifikapo 2030 Tanzania isiwe na maambukizi mapya ya Ukimwi ni vema Vijana na Wanaume wakajitokeza kuima ili kujua afya zao pamoja na kuanza kutumia dawa kwa usahihi kwa wale wanaogundulika kuwa na maambukizi.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaweza pia kufikiwa hata kabla ya muda huo endapo jamii na wadau wakajitokeza kutoa elimu na kuhamasisha kupima ikiwa ni pamoja na kuuqwezesha Mfuko wa kudhibiti Ukimwi kwa kuchangia fedha ili kuepukana na utegemezi.
Alisema hatua iliyofikiwa na tume juu ya mapambono ya Ukimwi ni makubwa lakini inakabiliwa na ukosefu wa fedha hivyo kila mwananchi anapaswa kuchangia chochote ili mfuko huo uepukane na kutegemea fedha za wafadhili ambazo zuina mwisho wake.
“Ili kufikia malengo tuliojiwekea ni lazima Tume iwe na fedha zake kupitia mfuko ulioanzishwa kwa wadau na wananchi mmoja mmoja kuchangia fedha kidogo kidogo kwani hadi sasa kazi waliyofanya hawa watu wa Tume ni kubwa sana” amesema Waziri Mkuu.
Aidha ameongeza kuwa njia nyingine ya kufikia malengo hayo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayezaliwa akiwa na maambukizi kuanzia sasa ili kuwa na kizazi salama kwa kutoa elimu kwa wanaume pamoja na akina mama kuanzia ngazi ya chini.
Awali akitoa maelezo kuhusu kongamano hilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tickson Nzunda amesema kutakuwa na wadau 150 pamoja na washiriki zaidi ya 500 ambao watajikita katika kujadili namna ya kufanya utafiti, utoaji wa huduma, kuhamasisha jamii, kutoa elimu na kutoa mwelekeo wa namna ya kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi ya Bunge, Fatma Toufiq alisema Kamati itaendelea kuishauri Serikali kutenga bajeti ya kutosha ili ifikapo 2030 Tanzania isiwe na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt.Leonard Maboko amesema Kongamano hilo ni la sita kufanyika tangu kuanzishwa kwake ambalo hufanyika kila wakati wa maadhimisho ya Ukimwi duniani ambapo wadau huja na mapendekezo na maoni yanayopaswa kufanyika.
Aliongeza kuwa katika kongamano hilo jumla ya mada 34 zitajadiliwa kwa mdomo kati ya Mada 57 zilizopo ambapo zinazobakiwa zitawasilishwa kupitia mabango mbali mbali yatakayowekwa ukumbini.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema katika Mapambano dhidi ya Ukimwi Serikali imetenga shilingi Bilioni 6.1 ka ajili ya wanasayansi kufanya utafiti wa Sayansi Tiba ili baadae wajikite kwenye uzalishaji.
More Stories
Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Kimataifa matumizi bora ya Nishati
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa