Na Projestus Binamungu,TimesMajira Online,MAELEZO
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuwashirikisha wadau wa lugha ya Kiswahili katika kuboresha Mkakati wa Taifa wa Miaka 10 wa Kubidhaisha Kiswahili ili uzinduluwe na kuanza kutekelezwa.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo jana katika kikao na Watendaji wa Baraza hilo kilichofanyika Ofisi za BAKITA Jijini Dar es Salam ambapo aliambatana na Naibu wake Pauline Gekul.
Pamoja na kuagiza ushirikishwa wa wadau katika kuboresha mkakati huo, Waziri Bashungwa pia ameiagiza BAKITA kufanya maboresho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufunguzi wa vituo maalum vya kufundishia lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali duniani.
Mkakati huo unaopendekezwa na BAKITA unalenga kubidhaisha lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2021-2031, ambapo lugha hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imeanza kutumika kama lugha rasmi katika nchi mbalimbali duniani na Jumuiya za Kimataifa kama Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC) na Jumuiaya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi, baada ya kupokea maelekezo viongozi hao, hatua inayofuata ni kuwapitisha wadau wa Kiswahili katika Mkakati huo kabla ya kuuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi, kwa ajili ya hatua zaidi za kiutendaji na utekelezaji wa mkakati huo.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda