November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ya wazawa kuwekeza kwenye sekta ya mafuta, gesi yaongezeka

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli(PURA), imesema kasi ya washiriki wazawa kuwekeza katika mnyororo Mkubwa wa mafuta na gesi umeongezeka kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa kitengo cha ushirikishwaji wa wazawa na uhusishwaji wa wadau kutoka PURA, Charles Nyangi katika maonesho ya 45 ya kimataifa ya Sabasaba.

Amesema, kasi hiyo imeongezeka pindi Mamlaka hiyo ilipoanza zoezi la kuhamasisha wazawa kuwekeza katika mnyororo Mkubwa wa mafuta na gesi na kufanya wazawa wengi kuwekeza.

“Ukiangalia kwa miaka ya nyuma upande huu wa washiriki wazawa ulikuwa ni mdogo mpaka Makampuni ya wawekezaji yalikuwa yanakuja na watu wao hadi wapishi lakini baada ya kuanzisha kwa PURA kwa kiasi fulani tumefanikiwa kuwezesha ushiriki wa wazawa kuongezeka,”.

“Mfano Kisima cha mwisho kilichochimbwa katika kina kirefu cha bahari kuu, ushiriki wa wazawa uliongezeka kutoka watano na mwaka huu kutoka katika kisima cha mwisho kuchimbwa wazawa walioshiriki walikuwa 56 ikiwa ni matokeo ya kuanzishwa kwa Pura na matokeo ya ushiriki kwa wazawa,”amesema kiongozi huyo.

Kupitia maonesho hayo, wamesema wanaendelea kuhamasisha washiriki katika kusimamia na kudhibiti mkondo wa juu wa petroleum na mradi wa usindikaji wa gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).

Amesema, PURA inasimamia na kudhibiti LNG na tayari utekelezaji wa mradi huo umeanza Mkoani Lindi na utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi kwa kutoa kutoa zaidi ya ajira 40000 kwa vijana kupitia mradi huo.

Amesema, kupitia mradi huo ambapo Waziri mwenye dhamana aliendesha mafunzo kwa wadau juu ya mradi huo huku serikali ikifufua mazungumzo kuanzia Agosti hadi Oktoba ambapo yatakamilika na kwenda katika hatua nyingine ya utekelezaji.

“Miradi ikija tunahitaji watanzania washiriki katika ajira,uwekezaji na kusambaza material na hadi sasa Maandalizi kwa upande wa serikali yameshaanza na timu nzima,”amesema.