Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dodoma
WAZIRI wa Madini,Dotto Biteko, amewahakikishia wawekezaji na wadau wengine wa sekta ya madini mazingira bora ya uwekezaji na kufanya biashara akisema hicho ni kitu muhimu kwa ustawi wa sekta hiyo na maendelo ya taifa kwa ujumla.
Waziri Biteko pia ameipongeza Benki ya NMB kwa kuwakutanisha wadau wa sekta ya madini na kuwapa fursa ya mafunzo ya biashara na kubadirishana mawazo kwa ajili ya ufanisi wao binafsi na kisekta kwa ujumla.
Biteko aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa “NMB Mining Club” ambalo ni jukwaa la kwanza nchini mahsusi la kuwahudumia wadau wa madini akisema uwezeshaji wao unawezekana.
“Kama mnavyojua, mlengo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya wafanyabiashara ili kuwawezesha kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia kodi, kutoa ajira na kuongeza mitaji.
“Tunaendelea na kusisitiza zoezi la kuongeza thamani ya madini lifanyike hapa hapa nchini ili taifa liweze kunufaika na utajiri wake mkubwa wa rasilimali hii na tayari Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi katika siku zake 100 za kwanza kwa ajili ya kuhakikisha hilo linafanikwa.
“Tumeshatoa leseni za usafishaji madini ya dhahabu nne ambapo tayari kiwanda kimoja kimezinduliwa Mwanza na mambo mengine mazuri yanakuja,” alisema Waziri Biteko.
Pia alisema “NMB Mining Club” ni ubunifu wa hali ya juu na kazi kubwa za aina hiyo ndizo zinaifanya benki hiyo kuwa kinara wa huduma na maarifa mapya sokoni. Kwa kuonyesha njia mpya ya kuwahudumia wachimbaji, NMB imetengeneza chanzo kipya cha mapato na kuwapata wateja wapya, alifafanua.
Alizichagiza benki nyingine kuiga mfano wa NMB na kuanza kuwakopesha kikamilifu wadau wa sekta ya madini na kuzitaka taasisi hizo kuunganisha nguvu kwa ajili ya kujenga uwezo wa kufadhili miradi mikubwa ya madini,
Klabu hiyo mpya inayojumuisha zaidi ya wadau wa madini 200 wa Kanda ya Kati imelenga kutoa mafunzo kuhusu maarifa ya biashara (elimu juu ya mipangilio ya biashara na elimu ya mwendelezo wa kitaalamu wa madini) na fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu wa kibiashara.
Wadau hao ni pamoja na wamiliki wa migodi, maduka makubwa ya vifaa vya uchimbaji, viongozi kutoka kampuni za madini, Kampuni ya Taifa ya Madini (Stamico), vyama vya wachimbaji wa kada zote na madalali.
Awali, Afisa Mkuu wa Mikopo wa NMB, Bw. Daniel Mbotto, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati biashara nyingi zikipata changamoto akitolea mfano wa kushuka kwa thamani ya bei ya Tanzanite kwenye soko la dunia.
Alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kusaidia ukuaji wa sekta ya madini kwa kuchochea shughuli za uchimbaji na hivyo kusaidia ongezeko la mapato ya serikali kupitia mrabaha, tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma.
“Kwa kutambua juhudi chanya za Serikali kuanzisha masoko 39 na vituo 50 vya kuuzia madini, Benki ya NMB imehakikisha huduma za kifedha zinapatikana karibu ya vituo na masoko ya madini jambo ambalo limerahisisha huduma kwa wateja wetu,” alisema Bw. Mbotto.
Kuhusu “NMB Mining Club”, Bw Mbotto alisema ni mpango unaolenga kufikia miji sita nchini yaani Mwanza, Chunya, Morogoro na Arusha, ukianzia Dodoma na Kahama na maeneo ya karibu kwa lengo la uwezeshaji na kutoa mafunzo ya biashara.
“Leo tunazindua mtandao huu wa wadau wa sekta ya madini na tunawakaribisha wasiokuwa wateja waweze kufungua akaunti na sisi ili waweze kuwa wanachama wakudumu wa NMB Mining Club,” alisema.
Huku akiwahakikishia wadau hao faida lukuki, Bw. Mbotto alisema Benki ya NMB imeendelea kuwa benki inayoongoza kwa faida kwa kupata Sh206 bilioni baada ya kodi mwaka 2020 na kuvunja rekodi ya faida kwenye sekta ya kibenki chini.
Naye Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Bw Alex Mgeni, aliiomba serikali kuisaidia benki hiyo kuwahudumia wachimbaji wadogo kwa kutatua changamoto zinazowakabili kama kukosa sifa za kukopesheka.
Alisema kwa mfano leseni zao zikitumika kama dhamana itakuwa rahisi kuwakopesha na kuwawezesha kifedha. Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula, alisema hilo linawezekana lakini lazima kwanza lifanyiwe kazi na kufuata taratibu stahiki.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa