November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA Shinyanga wasusia uchaguzi

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoani Shinyanga kimetangaza rasmi kutosimamisha mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Chona, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini hapa na Mwenyekiti wa CHADEMA, mkoani Shinyanga, Emmanuel Ntobi na kwamba hakuna mwanachama ye yote wa CHADEMA aliyejitokeza kuchukua fomu za kugombea kwenye uchaguzi huo kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Ntobi amesema chama chake hakiwezi kushiriki katika uchaguzi huo wa marudio kwa vile tangu awali kilishatangaza kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kote mwaka jana 2020 na pia hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Tunapenda kuutarifu umma kuwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, hakitashiriki katika uchaguzi mdogo wa marudio, ambao umetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanyika mwezi Julai 2021 katika kata ya Chona, Halmashauri ya Ushetu, Mkoa wa Shinyanga.

“Aidha, tunapenda kuutarifu umma mpaka sasa, Chama hakijafanya mchakato wowote wa ndani ya chama (utoaji fomu, kura za maoni) na wala hakuna kikao chochote cha Kikatiba cha ngazi yoyote kwa maana ya kata wala jimbo kilichoketi kupitisha mgombea udiwani katika kata ya Chona,” ilieleza sehemu ya taarifa ya CHADEMA.

Ntobi alifafanua kuwa katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, Toleo la 2019, Ibara ya 7.3.9 (a) na 7.4.10 (a) inaeleza wazi taratibu za uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali za kiserikali ambazo vyama vya siasa hutakiwa kusimamisha wagombea kwa mujibu wa Katibu ya nchi.

Hata hivyo Ntobi amesema CHADEMA imeshangazwa na taarifa za kuwepo mtu mmoja ambaye hafahamiki ndani ya chama, makazi wala anuani yake havifahamiki ambaye inasemekana ameghushi muhuri wa Chama, saini za viongozi na kwenda kuchukua fomu kwa Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi akiomba kuteuliwa kugombea udiwani kata ya Chona.

“Kwa hatua za awali, Chama tumekwisha muandikia barua rasmi Msimamizi Msaidizi wa kata ya Chona, barua yenye Kumb. Na. CDM/USHT/01/2021 pamoja na mambo mengine tumemtaka amuondoe mara moja mtu huyo kwenye orodha na asitumie jina na nembo za CHADEMA. Tumeazimia kutoshikiri uchaguzi wowote wa marudio mpaka tutakapopata Tume huru ya uchaguzi,” ilieleza taarifa.