Jokate akabidhi ofisi
Kisarawe akiacha alama
Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Kisarawe
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Jokate Mwegelo amekabidhi rasmi Ofisi ya Wilaya ya Kisarawe kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Nickson John Simon ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kuteua wakuu wa wilaya nchini.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Idara za Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakiongozwa na Mkurugenzi wao Mussa Gama pamoja na viongozi wa taasisi zilizopo ndani ya Wilaya hiyo.
Akizungumza wakati akikabidhi ofisi hiyo, Jokate ambaye amehamishiwa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam amesema anaondoka Kisarawe kiutendaji na kiutumishi, lakini moyo wake umeja upendo mkubwa wa wana Kisarawe ambao walimpokea, kumleta na kumfunda hadi kuendelea kuaminiwa tena na Rais Samia, hivyo kwake watabaki kuwa watu muhimu kwenye historia ya maisha yake.
“Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ndugu yangu, Nickson wewe ulishaonesha mahaba makubwa na Wilaya yetu na huenda Rais wetu ameona hilo ameamua kukuleta Kisarawe.Wananchi wa Kisarawe wana upendo mkubwa, Kisarawe mambo yote ya maendeleo yanawezekana.
Niwaombe ndugu zangu wana Kisarawe tumpe ushirikiano zaidi ule mliyokuwa mnanipatia mimi.
“Najua kuna muda lazima uwe mkali kwa maslahi mapana ya Kisarawe, kwa maslahi mapana ya Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla. Ndugu yangu Nickson wewe ndio usukani wa Wilaya ya Kisarawe, njoo na maono yako,njoo na ubunifu wako, sio lazima ufanye kama nilivyofanya mimi, kikubwa unatakiwa kuwa na mipango yako ilimradi Kisarawe iende mbele.
Unaye Mbunge mzuri Selemani Jafo, hana tatizo lolote, ameniwezesha kufanya ninachokiona kinafaa,ametuachia uhuru na ukweli namshukuru, nawe Nickson mshike mbunge wetu atakusaidia.
Binafsi niseme nawapenda sana Kisarawe mmenilea,mmenikuza na kunifanya niendelee kuaminika,”alisema Jokate.
Alifafanua Kisarawe ndio Wilaya yake ya kwanza kujifunza uongoza na hata alipokuwa anapita kwenye wakat mgumu kwa baadhi ya nyakati lakini wana Kisarawe waliendelea kumshika mkono na kumtia moyo.Nawashukuru sana Kisarawe.”Kubwa zaidi naomba nikabidhi ofisi kwako, na viongozi na wananchi mumpe ushirikiano”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Nickson Simon akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo, amesema amewaambia viongozi wa Wilaya hiyo na wananchi jambo kubwa ni kuendelea kushirikiana kwa lengo moja tu la kuleta maendeleo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye sasa amehamishiwa Wilaya ya Temeke, Nickson amesema kikubwa ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini kubwa zaidi wote kwa umoja wso watasonga mbele.
“Tukishirikiana kwa kila kidogo ambacho kila mmoja wetu anacho tukiunganisha tutakwenda mbali sana.Niseme tu Mkuu wetu wa Wilaya Jokate amefanya mambo makubwa na ameacha alama.Nami niahidi nitafanya zaidi ya alipofanya yeye maana amenionesha njia, nina mahali pakuzia pale alipoishia yeye.Mimi nimekuja na mambo matatu ambayo nitayasimamia kwa nguvu zangu zote ni ujuzi, sayansi na kuinua vijana kiuchumi kupitia biashara ndogo ndogo.
Hivyo amesisitiza maono yake kwa Kisarawe ni Ujuzi, Sayansi na kuinua wananchi kiuchumi na vyote hivyo vikifanyika watafanikiwa na kuvunja mzunguko wa umasikini kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.”Haya maono haya niliyonayo yatafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja.Ndoto yangu siku moja ni kuiacha Kisarawe ikiwa na ujuzi, yenye kuifahamu sayansi na uchumi wa wananchi hasa vijana uimarike.Kisarawe ni Wilaya kongwe,ni Wilaya ya wajanja na ndio maana ilikuwa ya kwanza kuwa Wilaya.”
More Stories
Rais Samia apeleka neema Tabora
Samia apeleka neema Tabora, aidhinisha Bil. 19/- za umeme
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka