Na Esther Macha,TimesMajira,online,Dodoma
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA),imeendelea kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji kwa kutumia vyanzo ambayo vitapatikana nje ya mji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA),Mhandisi Aron Joseph, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea Mamlaka hiyo kwa lengo la kufahamu mikakati ya uzalishaji maji ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa sasa.
Amesema hadi sasa mamlaka hiyo inahudumia wakazi zaidi ya 500000 na kwamba ili kukidhi mahitaji ya wananchi hao jumla ya lita milioni 103 zinahitajika, licha ya kuwa hadi sasa lita milioni 66 zinapatikana na hitaji likiwa ni lita milioni 37.
Amesema miongoni mwa mikakati waliyoiweka ni kuendelea kuchimba visima vya maji kwenye maeneo yaliyo nje na Jiji la Dodoma kwa lengo la kupanua wigo wa utoaji na usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
“Miaka 30 ijayo uhaba wa maji safi na salama katika Jiji la Dodoma itakuwa ni historia kwa sababu serikali imeanza kutekeleza miradi miwili mikubwa ikawamo chanzo cha Ziwa Victoria na bwawa la Falukwa, ambayo mbali na kuhudumia Jiji hilo pia maeneo ya jirani nayo yatanufaika,”alisema Mhandisi Joseph.
Aidha amesema kuwa katika mradi wa bwawa la Falukwa wanategemea kuzalisha lita 128 za maji kila siku na kwamba mradi huo unafadhiliwa na watu wa Marekani aliongeza kuwa kuhusu mradi wa Ziwa Victoria tayari usanifu wa awali ulikwishaanza na kwamba utapita katika Mkoa wa Singida hadi Dodoma.
Ameongeza kuwa idadi kubwa ya wananchi Jijini humo imechangia mifumo ya maji taka kuzidiwa na kwamba hadi sasa ni kilometa 116 sawa na asilimia 20 ya upatinaji wa mfumo wa maji taka.
Hata hivyo amesema Serikali imeona tatizo hilo hivyo imeongeza eneo la mfumo wa maji taka kupitia mradi unaofadhiliwa na Korea mkopo wa dola milioni 70 na utahudumia kilometa 250 za mfumo wa maji taka sambamba na kujengwa mabwawa yasiyopungua 16 na kuwafikia wateja wasiopungua 600.
Kwa upande wake Mhandisi wa uzalishaji maji DUWASA, Peter Shemwelekwa amesema jumla ya visima 21 vya maji vimechimbwa katika Jiji la Dodoma huku kituo cha kuzalisha maji cha Mzakwe kikitumika kuzalisha na kusambaza maji kwenye maeneo mbalimbali.
Amesema kituo hicho cha Mzakwe kinazalisha maji lita milioni 61.5 lakini hufikia uzalishaji wa lita 62 kwa siku endapo hakuna tatizo la umeme.
Mhandisi wa uendeshaji DUWASA, Emmanuel Mwakabole amesema miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha utaoji wa huduma ya maji kwa wananchi ni katizo la umeme ambalo huathiri mifumo ya kusafirisha maji pamoja na uharibifu wa miundombinu ikiwamo kupasuka kwa mabomba.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha