Na Mathew Kwembe, Mtwara
SERIKALI imeziagiza shule zote hapa nchini kutenga maeneo maalum yatakayotumika kwa ajili ya michezo na sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo kwa niaba ya Waziri Profesa Joyce Ndalichako wakati wa kufungua mashindano ya 41 ya Umoja wa Shule za Sekondari (UMISSETA) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaon mjini Mtwara.
Amesema, Wizara yake itahakikisha kuwa kila shule inakuwa na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya michezo ikiwemo michezo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kuboresha ufundishaji wa michezo kama vitalu vya vipaji na msingi wa ushiriki endelevu katika michezo kwa afya, elimu, uchumi na ajira.
Amesema kuwa, serikali imejidhatiti kuendeleza vipaji vya wanafunzi kupitia kufundisha somo la haiba na michezo kwa shule za Msingi na Elimu kwa Michezo kwa vyuo vya ualimu.
Naibu Katibu Mkuu aliongeza kuwa, kupitia wadhibiti ubora Wizara itahakikisha kunafanyika kwa tathmini na ushauri wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi.
Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA, Leonard Thadeo amesema, michezo yote iliyoshindaniwa wakati wa mashindano ya UMITASHUMTA itakuwepo isipokuwa mchezo wa mpira wa goli ambao haujaanza kushindaniwa katika shule za sekondari.
Michezo mingine itakayoshindaniwa katika UMISSETA ni pamoja na mchezo wa soka wavulana, na wasichana, netiboli, mpira wa mikono wavulana na wasichana, mpira wa wavu wavulana na wasichana, riadha wavulana na wasichana, mpira wa kikapu, na kwaya na ngoma katika sanaa za maonesho.
“Jumla ya wanafunzi 3200 kutoka Mikoa 28 ya Tanzania ikiwemo Mikoa miwili ya Tanzania visiwani (Zanzibar) wanashiriki mashindano haya ambayo itafanyika kwa siku 11 katika viwanja vya shule ya Ufundi na Chuo cha Ualimu Mtwara na tunatarajia yatakuwa na mafanikio makubwa,” amesema Thadeo.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship