November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kutumia fursa za uwekezaji wilayani Kahama

Na Patrick Mabula,TimesMajira Kahama

SERIKALI Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imetoa wito kwa wafanyabiashara kujitokeza kukitumia Kituo cha Biashara na Uwekezaji walayani hapa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kiweze kuwasaidia katika fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ushauri na elimu juu ya namna ya kuboresha bidhaa zao katika kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa juzi na mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alipokuwa akizindua maonyesho ya biashara kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa yatakayoanza rasmi kesho ambayo yatahusisha sekta binafsi na serikali, lengo likiwa kuwasaidia kupata masoko ya bidhaa zao.

Akizungumza na viongozi wa kituo hicho cha biashara na uwekezaji na wafanyabishara wa sekta mbalimbali za umma na za binafsi aliwataka wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kutumia kituo hicho cha biashara kilicho chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kutimiza malengo yao ya masoko na kuuuza bidhaa zao kiuchumi.

Macha amesema, kituo hicho cha biashara ambacho kipo chini ya ofisi ya waziri mkuu ni cha pekee na cha kwanza kufunguliwa hapa nchini wilayani Kahama kwa malengo ya kuwasaidia wafanyabiashara wakubwa kutimiza ndoto zao za kujikwamua kiuchumi aliwataka wakitumie kiwasaidie katika shughuli zao waweze kujiletea maendeleo na kusaidia kuchangia pato la taifa.

Amesema, Wilaya ya Kahama kuna fursa nyingi za kiuchumi hivyo aliwahimiza wakitumie kupata mafunzo, elimu na namna ya kuboresha bidhaa zao na kujitangaza waweze kupata masoko kwa sababu serikali inawatambua sana sekta binafsi katika kujenga uchumi wa taifa katika kujiletea maendeleo kwa ujumla.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo, Simon Cheyo amesema, maonyesho hayo yanayotarajia kufunguliwa kesho alisema wameyaandaa kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kukutana na kuonyesha bidhaa zao katika kuwasaidia kupata fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kaimu mkuu wa kituo cha biashara,Oscar Damasi amesema, ofisi ya waziri mkuu ilifungua kituo hicho chini yake toka mwezi Novemba, 2018 na kuna taasisi za serikali, umma na binafsi zinazohusika na kuwasaidia masuala ya biashara elimu, ushauri namna ya kuboresha bidhaa na shughuli zao juu ya kujipatia masoko.

Mwandaaji wa maonyesho hayo, afisa masoko wa kampuni ya GS 1, Shaban Mikongoti inayohusu kuweka alama ya utambuzi kwenye bidhaa amesema, lengo la kufanya maonyesho hayo hapo ni kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo hapo na namna ya kuweza kuwasaidia wafanyabiashra wadogo na wakubwa katika shughuli zao.