September 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apongezwa kukutana na wazee

Na David John, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MWANADIPLOMASIA na Naibu Katibu wa Baraza la Wazee Kata ya Kijichi Juliana Lubuva, amempongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kukutana na wazee na kupata fursa ya kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu ujenzi wa taifa.

Juliana amesema, Rais Samia alichokifanya ni kitu kizuri kwani kitendo cha kukaa pamoja na wazee na kujadiliana baadhi ya mambo ni hatua kubwa kwani amekuwa muwazi katika yale anayoyaamini kwenye serikali yake.

Akizungumzia hilo katika kikao lilichofanyika kwenye viwanja vya mlimani City Jijini Dar es Salaam Juliana amesema, Rais Samia amefanya jambo kubwa na lakupongezwa kwa kufafanua mengi juu ya mstakabali wa wazee.

“Rais Samia ametutendea haki wazee wa Dar es Salaam, kwaniaba ya wengine hapa nchini kwani hata katika hotuba yake unaona kabisa kwamba anachokiongea kinatoka moyoni kwake na si vinginevyo.

“Kuna haja kama taifa kurudi kwenye maadili kwani hivi sasa maadili yameporomoka sana na ndio maana leo hii kijana hawezi kumpisha Mzee kwenye vyombo vya usafiri Jambo ambalo huko nyuma halikuwepo,” amesema Juliana.

Juliana amesema, Rais Samia kama mwanamama jasiri na Mwenye mitazamo chanya kwa nchi yake na watu wake na ndio maana amekuwa mkweli hata kuelekea mabadiliko ambayo ametangaza kuyafanya ndani ya Serikali.

Alifafanua kuwa, katika kikao hicho wazee walikuwa na mahitaji yao ambayo wanataka watimiziwe ikiwa pamoja na asilimia 10 zinazotokana na mapato ya Halmashauri na wao waweze kufikiriwa kwani ni sehemu ya kundi maalum.

Pia uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi kama vile Bunge na mamlaka zingine ili na wao waweze kuwa na mtu wakuwasemea changamoto zao, lakini pia kwenye sekta ya afya wamesema bado hakujakuwa rafiki sana kwa upande wao.

“Kiukweli, Rais Samia ameonyesha kukubaliana na hoja karibu zote za wazee huku akihaidi kuzifanyia kazi siku za mbeleni na zingine tumemsikia akimwagiza Waziri wa afya kushughulikia haraka hususani kero zinazohusu afya,” amesema Juliana.

Amesema, kitu kingine ambacho kilimvutia ni jinsi Rais alivyokuwa muazi, amewaeleza wazee kuwa tayari na kuyapokea mabadiliko ambayo atayafanya siku si nyingi huku akisema anajua kuwa watoto wao wapo.lakini wawe wavumilivu.

Hata hivyo amesema, rais Samia amewaeleza kwamba kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa katika nchi ndio maana hata suala la kupandisha mishahara litafanywa hapo baadae huku akisisitiza kumaliza miradi yote ya kimkakati.