Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Sengerema
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele kulipa uzito suala la viwango, ubora na usalama wa bidhaa ili kuweza kuongeza tija.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Meneja Mafunzo na Utafiti wa TBS, Hamisi Sudi Mwanasala, wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya.
Mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 27, mwaka huu yalifanyika katika wilaya nne kwa nyakati tofauti za Kahama, Bukombe, Mji Mdogo wa Katoro, wilayani Geita na kuhitimishwa Sengerema.
Mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki zaidi ya 300 katika wilaya hizo.
Katika mafunzo hayo washiriki walipewa elimu kuhusu TBS na majukumu yake, kanuni bora za uzalishaji, matakwa ya viwango, namna bora ya uhifadhi, ufungashaji na teknolojia ya vifungashio na taarifa za msingi kwenye vifungashio.
Aidha, Sudi amesema washiriki hao walielimishwa juu ya taratibu za usajili wa bidhaa za vyakula, vipodozi na majengo, kazi ambazo hapo awali zilikuwa zikifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Kwa mujibu wa Sudi, Shirika hilo limeandaa mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kikao kilichofanyika Sirari,mkoani Mara, ambacho kiliridhia TBS,itoe mafunzo kwa wajasiriamali wanaosindika, kuzalisha, kufungasha na kuuza mchele katika kanda nzima ya Ziwa.
Amesema wametiwa moyo na mwitikio na ushirikiano mzuri walioupata katika wilaya zote za Kahama, Bukombe, Sengerema na Mji Mdogo wa Katoro, Geita wakati wa maandalizi ya mafunzo haya.
Amesisitiza kwamba mafunzo hayo ni uthibitisho wa azma ya Serikali katika kufanikisha malengo ya Tanzania viwanda.
“Na kwa sababu hiyo tuliona muelekeo mzuri wa usimamizi wa Serikali ya awamu ya tano ambao umeweza kututoa katika uchumi wa chini na sasa tumeingia uchumi wa ngazi ya kati na Awamu ya Sita Kazi inaendelea,” amesema.
Ametoa wito kwa watakaoupata mafunzo hayo waweze kuyatumia watakaporejea kwenye shughuli zao. Aliahidi kuwa TBS itaendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo kwa wazalishaji, wauzaji na wadau wote wa mchele.
Wakizungumzia mafunzo hayo, washiriki waliipongeza TBS kwa kutoa mafunzo hayo hasa kwa kuzingatia kwamba yametolewa wakati muafaka wa mavuno ya mpunga. Wametoa wito kwa shirika hilo kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea