November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC aingilia kati mgogoro wa vibanda Soko la Rebu

Na Timothy,Timesmajira Online. Itembe Mara

MKUU wa Wilaya Tarime mkoani Mara, Mtemi Msafiri ameagiza vibanda vya wafanyabiashara kuendelea kumilikiwa na waliovijenga, hadi mazungumzo yatakapofanyika baina ya wamiliki na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Mjini.

Hatua hiyo imekuja baada ya wafanyabiashara wa vibanda kufika ofisini kwake, kulalamikia kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime inawanyang’anya wamiliki vibanda na kuwasainisha mikataba wafanyabiashara kinyume cha utaratibu.

“Nimefuatilia ili kujua kama mna mkataba uliosainiwa baina ya wamiliki wa vibanda na Halmashauri ya Mji, ila nikaona hakuna mkaataba uliopo bali kuna rasimu ya mkataba ambao unasema, wamiliki watamiliki ambao ni wajenzi wake watatumia vibanda hivyo kutoka mwaka 2016 hadi 2031 huku halmashauri ikiwataka wamiliki hao, kutumia kuanzia mwaka 2016 hadi 2026 ambapo wote kwa pamoja wameingia mgogoro, mimi nasema mtaendelea kutumia vibanda vyenu hadi hapo mtakapokaa chini na Halmashauri ya Mji na kukubaliana,” amesema Msafiri.

Msafiri ameiwataka halmashauri kufungua vibanda vyote ambavyo vilivyokuwa vimefungwa na kuwataka kuendelea kutii maagizo anayoyatoa, huku wakizingatia kuwa yeye ni bosi wa wilaya si vinginevyo.

Kwa upande wake mmoja wa wamiliki wa vibanda vya soko la Rebu, Junya Mwera amesema awali halmashauri hiyo iliwapa rasimu ya mkataba Julai 2016 ambaye katika mkataba huo, atajulukana kama mpangaji kwa upande mmoja.

Naye Mariamu Maigga amesema baadhi ya wafanyabiashara wamefungiwa vibanda kinyume cha sheria ambapo wameshindwa kulipia watoto mahitaji ya shule kutokana na kushindwa kuifanyabiashara.