Na Esther Macha,TimesMajira,Online,Mbarali
MBUNGE wa Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya, Francis Mtega, ametoa zawadi zenye thamani ya shilingi milioni tano kwa ajili ya kuwapa motisha walimu 67 wa shule za msingi na sekondari waliowasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Mtega ametoa zawadi hizo jana,wakati alipotembelea baadhi ya shule kugawa zawadi kwa walimu hao 67 na kukabidhi madawati 875 aliyoyatoa kwenye shule nane mpya za Sekondari wilayani humo.
Amesema utoaji wa tuzo hizo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo alisema akipata ridhaa ya kuchaguliwa atatoa zawadi kwa walimu watakaofaulisha watoto pamoja na wanafunzi watakaofanya vizuri kwenye mitihani yao.
“Niliahidi kuboresha elimu wilayani humu na sasa natekeleza kwa vitendo nawashukuru walimu, watumishi wa Idara ya Elimu na wanafunzi na madiwani na watendaji kwa kutimiza wajibu wenu ipasavyo kiasi cha kunishawishi kutoa shilingi milioni tano kwa ajili ya motisha,” amesema Mtega.
Ameongeza kuwa Wilaya ya Mbarali inahitaji umoja na mshikamano ili kuongeza ufaulu kwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri kuanzia ya darasa la nne hadi kidato cha nne nchini.
Ofisa elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ,Anna Shitindi alisema kuwa zawadi hizo zilitolewa kwa makundi matatu ambayo ni walimu wa sekondari 55 na Msingi 16 ambapo jumla yake ni 67 na wanafunzi waliopata tuzo za kufanya vizuri ni wawili .
Amewaomba walimu kupitia motisha hizo kuongeza juhudi na ari ya ufundishaji ili kuhakikisha Wilaya inafanya vizuri.
Naye Ofisa Elimu shule za Msingi wilayani humo.Protas Mpogole amesema kuwa kutokana na nguvu alizowekeza mbunge ni vema kuongeza juhudi katika kufanya vizuri .
“Hili ni deni kwenu walimu nawaomba ndugu zangu walimu tuondoe halmashauri kutoka nafasi ya sita na saba hii wilaya kila mwaka inashika nafasi ya saba na sita naomba sasa kwa kushirikiana viongozi wa kata na uongozi wa wilaya naomba tuondokane na hizo nafasi inawezekana Mkoa ukawa unaongoza kwa mapato sasa kwanini kusiwe na uhusiano kati ya utoaji elimu?alihoji Mpogole.
Mmoja wa walimu waliopata zawadi hizo kutoka sekondari ya Herring Christian, Sijali Kayuni alimuahidi mbunge Mtega kuongeza bidii katika ufundishaji na kwamba imewathamini na kuwatia moyo hivyo ufaulu utaongezeka.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea