November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkoa wa Singida wazindua wiki ya chanjo

Na Dotto Mwaibale,Timemajira Online. Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amewataka wataalamu wa afya mkoani hapa kuchanganua na kuainisha hadharani ni kwa namna gani chanjo zinazotolewa, zimekuwa na tija kwa jamii ili kuleta msukumo kwa watu kuzipenda, kuzithamini, kuziheshimu na kuendelea kuchanjwa.

Akizindua ‘Wiki ya Chanjo’ kimkoa kwenye viwanja vya Kata ya Muhintiri wilayani Ikungi mkoani hapa, Nchimbi amewataka wataalamu hao kufuatilia na kutangaza hadharani matokeo na mazao ya chanjo hizo katika uhalisia wa maisha ili watu wajue.

“Wataalamu msikae kimya, tuelezeni mara kwa mara manufaa ya hizi chanjo ni kwa namna gani zimekuwa chanzo cha afya bora na akili timamu kwa ukuaji stahiki wa watoto wetu, vijana, jamii na taifa…tuelezeni zinavyochangia ongezeko la ufaulu mashuleni na manufaa yake kwa ukuaji wa uchumi,” amesema na kuongeza;

“Mkieleza vizuri ubora wa chanjo hizi kwa jamii na tukawaelewa, basi ubora huo ndiyo utakuwa msukumo katika kuchochea zaidi kasi ya ongezeko la watumiaji wake”.

Hata hivyo amesisitiza haitakuwa na maana yoyote kama chanjo zinazotolewa hazitaenda sambamba na lishe bora, huku akitumia nafasi hiyo kuhamasisha jamii kuzingatia vyote kwa pamoja, ili kuleta ustawi wa afya ya jamii kwa matokeo ya taifa bora.

Nchimbi amesema Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha juhudi zilizopo za utoaji wa chanjo zinakwenda sambamba na maboresho katika utoaji wa huduma nyingine za afya, ili kupunguza vifo visivyo vya lazima na kumlinda kila Mtanzania dhidi ya maradhi ambukizi.

Amewahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao, wanapata dozi nzima ya chanjo zinazotolewa kwenye vituo vya afya kwa kuzingatia chanjo ni chanzo cha afya bora na kinga madhubuti dhidi ya magonjwa hatarishi.