Na Omary Mngindo,Timesmajira Online. Kibaha
SERIKALI imeendelea kuwaonya watumishi wa serikali wanaoedelea kuwa kikwazo kwa wawekezaji, wakitakiwa kuacha mara moja tabia zao zinazoleta usumbufu kwa wenye dhamira ya kuwekeza.
Onyo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa baada ya kujionea mabasi mawili ya kubeba abiria yanayoundwa na Kiwanda cha BM Motors kinachomilikiwa na mzawa, Jonas Nyagawa kilichopo Kibaha Mji mkoani Pwani akiwa katika ziara ya siku moja.
Amempongeza Nyagawa kwa uwekezaji huo wa uundaji wa mabasi ambayo tayari mawili ameshayauza Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), huku akisisitiza kwamba anatamani kuona kampuni hiyo ikitengeneza mabasi zaidi na kuyauza hapa hapa nchini.
“Nimesikia taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo ikieleza kuwa BM Motors inaweza kulisha mabasi ya mwendokasi na kwamba unahitaji mtaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya kufanikisha hilo, nikuombe utumie fursa ya uwepo wa taasisi za kifedha kukopa kwa ajili ya malengo,” amesema.
Amemtaka mwekezaji huyo kama kuna changamoto yoyote awasiliane na Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa kisha kufika kwao ili kuzipatia ufumbuzi na kwamba
serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imewapatia magari mapya kwa ajili ya kazi hiyo.
“Nikuombe uongeze wigo wa uundaji wa mabasi ili makampuni na taasisi nchini, ziweze kuja kununua hapa badala ya kuagiza nje ya nchi hata mimi mwenyewe nikifanikiwa kupata pesa, naweza kuja kununua nilipeleke Rwangwa mkoani Lindi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Ndikilo ameiomba serikali kuongeza fedha Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), iweze kuweka lami kilomita sita katika eneo hilo lenye viwanda ambapo tayari imeidhinishiwa sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya kutengeneza kipande cha kilomita moja kwa kiwango cha lami.
“Nimeambiwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA kuwa, TAMISEMI imeiongezea sh. bilioni saba katika bajeti ya 2021/22, hivyo watajenga kwa kiwango cha lami kilomita sita kama ni kweli kipande hiki kitajengwa na kikiwa imara, hivyo kurahisisha wawekezaji kutumia kuleta malighafi na kusafirisha bidhaa,” amesema.
Awali Mkurugenzi Nyagawa ameelezea kufurahishwa kwake na ziara ya Waziri Mkuu, ikiwemo agizo lake la kuwataka wataalamu kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji huku akisema, milango yake ipo wazi na kuwa popote watakapokwamishwa wasisite kuwasiliana na ofisi yake ili hatua zichukuliwe.
“Ujio wa Waziri Mkuu siku chache zilizopita zimetusaidi kwani vibali vyote tumevipata, hivi sasa tuna kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu, tunaishukuru serikali kwa kutupatia fursa wawekezaji katika kufanikisha kwenye sekta hii,” amesema.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania