Na Judith Ferdinand,TimesMajira online,Mwanza
WITO umetolewa kwa wananchi kukubali na kuthamini vivutio ambavyo taifa limejaliwa kwa kuvitembelea na kuviona ili kutangaza,kukuza utalii na pato la taifa.
Pia Watanzania wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya biashara,utalii na uwekezaji ‘Tanzania Business Summit’ yanayotarajiwa kuanza Aprili 30 hadi Mei 2 jijini Mwanza,kwa kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani katika hifadhi ya taifa ya Kisiwa cha Saanane,makumbusho ya Bujora pamoja na hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa Cha Saanane,Acc.Eva Malya, ameyasema hayo wakati akizungumza na Gazei la Majira mkoani Mwanza, amesema mwitikio wa Watanzania kufanya utalii wa ndani bado ni mdogo hivyo Watanzania wakubali na kuthamini vivutio vizuri ambavyo Mungu ametujalia katika nchi yetu.
“Tuna vivutio na hifadhi nzuri Mungu ametujalia lakini kusema tu kwamba tunavyo haitoshi lakini tuwe tunakwenda kuvifaidi kwa kutalii na kuviona kwani kwa kutalii kwanza itasaidia kuvitangaza zaidi,kuvitambua.
“Pia kuvifurahia lakini pia itainua utalii wetu kama tunavyojua kuna nchi nyingine utalii wa ndani upo juu naamini tukiweka nia tutafanikiwa kuinua utalii wa ndani,nipende kuhamasisha kwa kuwaomba Watanzania kuvithamini vivutio tulivyopewa kwa kuviona na kuvitembelea,” amesema.
Sanjari na hayo amesema, katika maonesho ya biashara,utalii na uwekezaji watakuwepo kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani na kuratibu safari za Watanzania kutalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane kwa siku zote tatu za maonesho hayo, kutakuwa na safari nyingine ya kuelekea Bujora na Serengeti na safari hizo muhimu zitakuwa zinaanzia kwenye uwanja wa Rock City Mall kupitia katika vivutio ambavyo vipo katika Jiji la Mwanza.
Amesema kwa safari za Saanane gharama ni 13,000 kwa watu wazima,6,000 kwa watoto ambao ni kati ya miaka 5-15 na watoto chini ya miaka mitano ni bure gharama hizi zinajumuisha tozo ya hifadhi ya taifa ,tozo ambazo zitatozwa sehemu ambazo watapita za vivutio kama pale jiwe la Bismarck pamoja na maeneo ya makumbusho ya Kageye.
“Simba wetu ambao wapo katika kisiwa cha Saanane wamezaa watoto watatu kwa hiyo watalii wetu watapata fursa ya kuwaona hao watoto wakiwa katika mazingira ya kupendeza pamoja na wanyama wengine kama nyumbu,pundamilia,swala,ndege,mandhari ya kipekee ya uoto wa asili ya kuvutia,” amesema.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea