November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waridhishwa na usafishwaji eneo la Mradi wa JNHPP-MW2115

Na John Bera, TimesMajira Online

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imefanya ziara katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Mikumi kukagua maendeleo ya kazi inayoendelea kufanywa na kikosi kazi cha operesheni umeme kwenye Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP-MW2115) mkoani Morogoro.

Kamati hiyo imeridhishwa na kazi ya usafishaji wa eneo la mradi huo ambapo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema Wizara ya Maliasili na Utalii katika mradi huo ni mlengwa kwa kuwa eneo ambalo mradi unatekelezwa ni hifadhi.

“Tumetoa eneo kubwa ambalo lilikuwa Hifadhi ya Nyerere, sisi ni wadau wakubwa wa eneo hili,”amefafanua Naibu Waziri Masanja.

Amesema, pamoja na kutoa eneo hilo bado wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa shughuli za kusafisha maeneo yote ya mradi huo.

“Tumefika katika kambi hii ambayo inasimamiwa na jeshi wamesafisha eneo kubwa na kwa asilimia 57 wameshatekeleza imebaki kama asilimia 43,kamati imekuja kuangalia utekelezaji na hasa usafishaji wa eneo hili ambapo miti inayokatwa inachakatwa ili kupatikana mbao na kuuzwa kwa wadau mbalimbali na fedha kuingizwa kwenye mfuko wa Serikali,”amesema Naibu Waziri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Aloyce Kwezi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo alipongeza kazi kubwa inayoendelea kufanyika katika eneo hilo huku akiuelezea mradi huo kuwa sehemu ya utalii, hivyo Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuandaa miundombinu mizuri kwa ajili ya utalii.

“”Nawapongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya pia watumishi wa TANAPA,TAWA na TFS na wizara nzima, tumeridhishwa na maendeleo ya zoezi hili kupitia operesheni umeme ambalo limefikia asilimia 57,”amesema Dkt.Kwezi.

Ametoa wito kwa wizara zinazohusika na mradi huo kushirikiana kwa pamoja ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.