November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa ufuta, mbaazi wataka korosho iuzwe Namtumbo

NA Yeremias Ngerangera,Timesmajira Online. Namtumbo

KIKAO cha wadau wa mazao ya ufuta, mbaazi na soya kimependekeza zao la korosho linalolimwa kwa wingi katika Wilaya ya Namtumbo, nalo liuzwe wilayani hapa katika Chama Kikuu cha SONAMCU.

Akizungumza katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Magazini, Grace Kapinga amesema zao la korosho linalolimwa kwa wingi wilayani hapa na kwenda kuuzwa Chama Kikuu cha Wilaya ya Tunduru, inaikosesha Halmashauri mapato yake na kuleta usumbufu kwa wakulima hasa inapotokea changamoto kwenye malipo ya wakulima hao.

Awali Kaimu Ofisa Kilimo na Ushirika Wilaya ya Namtumbo, Astery Mwinuka ametoa taarifa ya utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta, soya na mbaazi kwa msimu wa 2019/20 na mapendekezo ya utekelezaji kwa msimu wa 2020/21 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Evance Nachimbinya.

Katika mapendekezo hayo tozo ya sh. 17 kwa kilo kwa ajili ya vifungashio, ambayo ilikuwa analipa mkulima imehamishiwa kwa mnunuzi pamoja na ushuru wa halmashauri ambao awali, wakulima walikuwa wanakatwa sh. 78 kama ushuru wa halmashauri nayo imehamishiwa kwa mnunuzi.

Hata hivyo mapendekezo ya tozo kwa msimu 2020/21 kwa mazao ya ufuta, mbaazi na ufuta yalipitishwa huku wadau wakitaka zao la korosho linalolimwa wilayani hapa kuuzwa pia Namtumbo likisimamiwa na Chama Kikuu cha SONAMCU.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Kizigo ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao amesema, suala la kuuzia zao la korosho wilayani hapa ni maamuzi ya pamoja hivyo kila mdau aliyehudhuria kikao hicho, kusimamia maamuzi ya kikao na si vinginevyo.

Naye Meneja Shughuli wa SONAMCU aliyehudhuria kikao hicho, Zamakanaly Komba amewathibitishia wadau kuwa chama hicho kitasimamia ukusanyaji, upimaji na uuzaji wa zao la korosho kama mazao ya ufuta, soya na mbaazi bila wasiwasi.