Na Nathaniel Limu,TimesMajira online,Singida
KANISA la Pentekoste (FPCT), Singida Mjini Kati,chini ya mradi wake wa Uwajibikaji katika jamii,limetoa mafunzo juu ya mapambano dhidi ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni,kwa makundi mbalimbali ikiwemo la viongozi wa dini na wa serikali.
Lengo la mafunzo hayo,ni kuyajengea uwezo makundi hayo ili yaweze kuwa mabalozi wazuri katika uielimisha jamii juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.Ili waweze kuyachukia na kuacha kuyaendeleza.
Akizungumza juzi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo,askofu mstaafu wa kanisa la FPCT,Dkt.Paulo Samwel,amesema kanisa limeamua lisibaki kuhudumia wakristo tu,mbali lisaidie jamii nyingine, ili iweze kushiriki kikamilifu kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.
“Pamoja na kutoa huduma ya kiroho,tumepanua wigo kwa kutoa mafunzo haya ili jamii iweze kushirikia au kuwajibika,kukomesha vitendo visivyokubalika mbele ya Mungu.Pia vipo kinyume na haki za binadamu,” alifafanua na kuongeza;
“Leo tupo hapa makundi mbalimbali.Wapo viongozi wa madhehebu ya dini, walimu,mahakimu,watendaji wa Serikali na wandishi wa habari.Kupitia makundi haya,nina uhakika tutatoka na mikakati itakayotuwezesha kukomesha vitendo hivi ambavyo vinachangia watoto wetu washindwe kufikia ndoto zao” amesema.
Aidha,Dkt.Samweli amesema wakazi wa Manispaa ya Singida wakishirikiana kwa pamoja,manispaa itapaa kimaendeleo kwa haraka zaid.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo raia kutoka Kenya,Njoroge Kimani,ametaja baadhi ya madhara yatokanayo na mimba za utotoni,kuwa ni mhusika kukatisha mwanafunzi n kupata haki yake ya elimu.
“Kwa ujumla maisha yake yatabadilika na kuwa duni na kupata kazi itakuwa ni shida.Sio yeye tu atakayeathirika,itaathirika familia,jamii na taifa litaathirika.Tatizo lingine linalowakabili watoto wa kike,ni ndoa za utotoni.Moja kati ya watoto wa kike watatu Tanzania,anaolewa kabla ya kufikisha miaka 18.Hili ni tatizo la kupigwa vita na jamii yote”,amesema Joroge.
Naye mkuu wa shule ya sekondari ya Kindai,mwalimu Scholastica Massawe,amesema baadhi ya wazazi/walezi Manispaa ya Singida,ni chanzo cha mimba za utotoni.
“Wazazi hawa kwa ujumla hawawajibiki kwa watoto wao.Baadhi ni walevi wa kupindukia na wengine mke na mume kupingana mara kwa mara.Vitendo hivyo vinasababisha wasione umuhimu wa kuwasapoti watoto wao katika masuala ya elimu.Mwanafunzi anaanza kidato cha kwanza hata hasindikizwi na mzazi.Utamaduni huu sio mzuri kabisa”,amesema mwalimu huyo kwa masikitiko.
Amesema wazazi hao wanawapa watoto uhuru mpana wa kupitiliza,kitendo kinachochangia wapate mimba utotoni.
Ameongeza kwa kusema wazazi wa Manispaa ya Singida,ni tofauti na wale wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni.
Mwalimu Massawe amesema upo umuhimu mkubwa wazazi wakaelimishwa na kuhimizwa kujenga utamaduni wa kusimamia maendeleo ya masomo ya watoto wao kwa njia hiyo,ufaulu utaongezeka.
Wakati huo huo,Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Singida,Dora Simion,amesema vitendo vya ushoga na vile vya kufanyiana kinyume na maumbile,vinaendelea kushamiri.
Amesisitiza kwamba elimu juu ya madhara ya vitendo hivyo ambavyo havikubaliki mbele ya Mungu na jamii,ikatolewa.Pia amependekeza nyumba za ibada ziangalie uwezekano wa kuanzisha madawati ya ukatili wa kijinsia.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea