November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuondoa wanufaika watakaotumia ovyo ruzuku

Na Veronica Mwafisi,TimesMajira Online. Momba

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amesema serikali haitosita kuwaondoa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini watakaoshindwa kutumia vyema ruzuku wanayopewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ili kuboresha maisha yao kama ambavyo serikali imekusudia.

Ndejembi amesema hayo akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mpango huo katika Vijiji vya Msangano, Nkala na Chiwanda wilayani hapa na kuongeza kuwa baada ya mwaka mmoja atarejea kujiridhisha kama fedha za ruzuku zilizotolewa kwa kaya maskini, zimetumika vizuri kuboresha maisha hivyo kaya zitakazobainika kutumia tofauti na malengo zitaondolewa kwenye mpango.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mnufaika, kutumia ruzuku anayoipata katika shughuli zitakazomuongezea kipato kama kilimo na ufugaji, ili kuboresha maisha yake na kuongeza kuwa Maofisa Ugani wana jukumu la kuhakikisha wanawasaidia wanufaika kufuga na kulima kisasa.

Amewataka wanufaika kuhusu ruzuku wanayoipata kuwa si kwa ajili ya anasa kwani serikali, inatoa kwa kaya maskini ili kuziwezesha kujikwamua kwenye lindi la umaskini.

“Serikali inatoa fedha kwa kaya maskini ili ziweze kujishughulisha na ufugaji, kilimo na ujasiriamali na baada ya muda ziweze kuondokana na umaskini,” amesema.

Kuhusiana na Kijiji cha Msangano ambacho hakijanufaika na mpango huo toka uanze, Ndejembi amewaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa ifikapo Julai mwaka huu kaya maskini kijijini hapo, zitaanza kunufaika na TASAF.

Amewataka Watendaji wa Serikali, kutokata fedha za ruzuku za wanufaika kwa ajili ya kuchangia huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na michango mingine, kwani fedha hiyo ni yake kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Ndejembi amesisitiza kuwa, kama kuna mchango wowote ni wa hiari hivyo si lazima akatwe ruzuku yake na kuongeza kuwa mnufaika, apewe fursa ya kuitumia fedha kujiendeleza kiuchumi katika ufugaji au kilimo ili akifuga na kuvuna achangie kwa hiari yake mwenyewe.

Amewahakikishia wananchi wa Vijiji vya Msangano, Nkala, Chiwanda na maeneo mengine kuwa, serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuzijali kaya maskini kwa kuzipatia ruzuku, hivyo amezitaka kutumia vizuri ruzuku hizo ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.