Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Mvumbuzi wa kanda za kaseti aliyepata sifa na kutambulika kwa teknolojia hiyo ambayo ilitumika kuhifadhi muziki, Lou Ottens amefariki dunia akiwa nyumbai kwake katika mji wa Duizel nchini Uholanzi mwishoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa mtandao wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Lou Ottens raia wa Uholanzi amefariki akiwa na umri wa miaka 94.
Inakisiwa kuwa zaidi ya kanda bilioni 100 zimeshauzwa duniani tokea teknolojia hiyo ilipoanza kutumika miaka ya 1960. Huku ubunifu wa Ottens ulifanikiwa kubadilisha kabisa namna watu walivyo sikiliza muziki, japo kaseti hazifanyi vizuri sokoni katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ujio wa teknolojia mpya za Compact Disk (CD), ambayo na yenyewe iko njiani kutoweka kutokana na ujio wa teknolojia ya flashi.
Ottens, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Philips mwaka 1960, pamoja na timu yake walitengeneza kwa mara ya kwanza mikanda ya kaseti ambapo mwaka 1963, kanda hizo zilitambulishwa katika maonesho ya Redio jijini Berlin na hatimaye kufanya vizuri duniani.
Hata hivyo, Ottens aliingia makubaliano na makampuni ya Philips na Sony ambapo kaseti ilipata hatimiliki, na baadaye baadhi ya makampuni ya Kijapani kuanza kuzalisha kwa idadi kubwa.
Hakuishia hapo, kwani alishiriki pia kutengeneza teknolojia mpya ya CD ambapo zaidi ya cd milioni 200 zimeshauzwa duniani mpaka sasa. Mwaka 1982, kampuni ya Philips ilipotengeneza mashine ya kucheza CD, Ottens alisema “kuanzia sasa, mfumo unaotumika kusikiliza muziki umefikia mwisho,”.
Miaka minne baadaye Ottens alistaafu. Alipouliza kuhusu fani yake, alisema masikitiko yake makubwa ni Sony ilitengeneza kifaa maarufu cha Walkman za kaseti na sio kampuni ya Philips.
Kanda za kaseti zilipoteza umaarufu miaka ya hivi karibuni, ambapo baadhi ya wasanii wa kizazi kipya wametumia teknolojia ya kanda za kasambaza miziki yao ikiwa ni pamoja na Lady Gaga.
Kwa mujibu wa makampuni ya muziki nchini Uingereza, mauzo ya kaseti yamepanda kwa asilimia 103 mwaka 2020 ukifananisha na miaka ya nyuma, wakati nchini Marekani kwa mujibu wa kampuni ya Muziki ya Nielsen, mauzo ya kanda za kaseti yaliongezeka kwa asilimia 23, na mwaka 2018 ikifananishwa na mwaka 2017.
More Stories
Mzee wa Bwax afunika ‘Kitaa food Fest’ Mbagala
TBL yazindua Kampeni ya ‘Smart Drinking’
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho