November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaagiza VIKOBA visajiliwe katika mfumo mpya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Pwani

SERIKALI imevitaka vikundi vidogo vya fedha vya jamii maarufu VIKOBA kujisajili katika mfumo mpya kabla ya Aprili 30,mwaka huu.

Hayo yamesemwa mkoani Mtwara na Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Zahara Msangi wakati ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Mtwara na Pwani.

Amesema, vikundi visivyosajiliwa kabla ya Aprili 30, mwaka huu havitaruhusiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Lengo la mfumo huu ni kuweka mwongozo mfumo wa usajili wa vikundi vya huduma za jamii ndogo za kifedha,”amesema Msangi.

Amesema, TAMISEMI inasimamia mamlaka za serikali za mitaa zinazotekeleza sheria ambayo imeagiza vikundi hivyo visajiliwe kwa mamlaka hizo vikiwa na watu wasiopungua 10.

Amesema, Septemba mwaka jana TAMISEMI ilivitaka vikundi hivyo vianze kujisajili kwa sababu awali vilikuwa vinajisimamia vyenyewe ndipo serikali ikaja na sera na kuwa sheria.

“Kama vikundi hivyo havitasajiliwa kwa mijibu wa sheria ifikapo Aprili 30,mwaka huu, havitaruhusiwa kufanya kazi hivyo nawaagiza maofisa maendeleo ya jamii mkimaliza mafunzo hakikisheni vikundi hivyo vinasajiliwa ili serikali iweze kutoa huduma bora kwa jamii,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Jerry Sabi amesema lengo la BoT ifikapo Machi 15,mwaka huu, mafunzo hayo yawe yametolewa kwa maofisa ustawi wa jamii wote nchini ili kuweza kuanza kivisajili vikundi hivyo.

“Tumegawa mafunzo hayo katika kanda tano nchini na tumeanza Mtwara kwa sababu walidai wamesahaulika na wanamazao yanayowapatia kipato kikubwa kama Korosho, “amesema.

Amesema kuwa kikundi kisichosajiliwa kitakuwa kimefanya kosa la jinai na kitafungwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Dunstan Kyobya amewataka maofisa maendeleo hayo kuwashirikisha elimu waliyoipata watendaji wote wa kata, mitaa, vijiji, vitongoji kwa sababu ndipo vikundi hivyo vinapoishi.

“Sitegemei kuwaona maofisa maendeleo mkikaa ofisini bali wafuateni watendaji hao ili kuwaeleza jinsi mfumo unavyofanya kazi na sitegemei kusikia visingizio,”amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum wa Mtwara Vijijini, Anastazia Wambura aliiomba BoT kuweka utaratibu wa kuziongezea halmashauri fedha kwa ajili ya kuvisaidia vikundi hivyo.

“Fedha za asimilia 10 za halmashauri hazitoshi na BoT msipoweka utaratibu wa kuzisaidia mtasababisha mgogoro wa kimaslahi kwa vikindi hivyo,”amesema.