November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania washauriwa kutembelea vivutio vya ndani vya utalii

Na John Bera, Mwanza

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mary Masanja amesisitiza kuwa fursa zilizoko kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii zikitumika ipasavyo zitasaidia kukuza Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mwenyekiti wa Kikao cha Pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Bw. Emmanuel Kipole wakati wa Kikao cha Bodi hiyo kilichofanyika Jijini Mwanza.

Masanja ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati wa kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa Mwaka 2020/2021.

Amesema, takwimu za watalii wanaoingia hapa nchini kuanzia mwaka 1993 walikuwa 230,000.

Aidha, mwaka 2019 idadi hiyo ya watalii iliongezeka na kufikia milioni 1.5.

‘’Idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 60, lakini ukingalia takwimu hizo watalii wanaoingia kwenye hifadhi zetu kuangalia vivutio ni milioni 1.5, hii inaonesha sisi Watanzania tuna kazi kubwa ya kufanya, kuwa wazalendo na kupenda vile tulivyo navyo,”amesema Masanja.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (Wapili Kulia)  akipitia baadhi ya Nyaraka za Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza akiwa pamoja na viongozi Mbalimbali wa mkoa wa Mwanza wakati wa Kikao cha Pili cha Bodi ya barabara ya Mkoa huo kwa mwaka 2020/2021 Jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, Mary Masanja amewaeleza viongozi wa mkoa huo kuwa uwepo wa vivutio vingi vya utalii katika Kanda ya Ziwa ni fursa pekee ya wananchi kuendelea kunufaika akitoa wito kwa viongozi waliohudhuria mkutano huo wahamasishe utalii wa ndani kwa nguvu zote.

“Ni lazima tuongeze nguvu katika kuhamasisha utalii wa ndani bila kusahau kuhamasisha wageni kutoka nje ya nchi yetu , Utalii wa ndani unatuhusu sisi wenyewe ,nikiuliza hapa wangapi wamefika kwenye hifadhi zetu na kwenye vivutio mbalimbali tulivyonavyo tutabaini idadi kidogo sana, nawaomba sana tuhamasishane,”amesisitiza Masanja.

Ameongeza kuwa, janga la Corona limesababisha kuyumba kwa sekta Utalii duniani kote pia hapa nchini kwa kuwa watalii waliokua wakitegemewa nchi zao zimeathiriwa na Corona hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa Balozi wa kutangaza Utalii na kutembelea vivutio vilivyopo.