November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi waonywa kujisadia vichakani

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Pwani

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba amewatahadharisha na kuwaonya baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuachana na vitendo vya kujisaidia vichakani, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa ya kutokea mlipuko wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mikakati waliyojiwekea ngazi ya mkoa katika kupambana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwenye maeneo mbalimbali hususan katika mkusanyiko wa watu wengine kama shuleni.

Kamba amesema kipindi hiki ni muhimu viongozi wa shule na mamlaka zinazohusika kuhakikisha wanazingatia maagizo yanayotolewa na wataalamu wa afya, ikiwemo kuzingatia usafi wa mazingira na kuweka mafi safi na salama katika maeneo ya shule, ili wanafunzi wanapotoka kujisaidia waweze kusafisha na kunawa mikono yao kwa lengo la kudhibiti mlipuko ya magonjwa hayo.

Ameongeza kuwa katika kupambana na wimbi la mlipuko wa magonjwa, wanaendelea kushirikiana bega kwa bega na walimu wa shule za Mkoa wa Pwani kuwaelimisha umuhimu wa usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi na kuwapa mafunzo, yatakayowasaidia kuwaelimisha watoto kujikinga na magonjwa yanayotokana na uchafu.

“Suala la baadhi ya wanafunzi, au jamii yoyote kuwa na tabia ya kujisaidia katika maeneo ya vichakani hii si sahihi hata kidogo, kwani ni hatari zaidi kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kama kuumwa na tumbo, kuhara na kipindipindu na kitu kingine mtu anaweza kujisaidia na mvua ikaja kunyesha, hivyo maji yakisomba kinyesi kunaweza kuleta madhara makubwa katika jamii ambayo ipo karibu na maeneo hayo.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano lengo lake kubwa ni kuhakikisha inaboresha sekta ya afya na kuwapa matibabu wananchi wake, hivyo isingependa kuona magonjwa ya mlipuko yanayoweza kudhibitiwa endapo jamii ikizingatia kanuni na taratibu zote, ambazo zinatolewa na watalaamu wa sekta ya afya ili kuondokana kabisa na hali hiyo.