November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu wakagua mradi wa kuzalisha Umeme wa Maji ya Mto Ruhudji

Na Zuena Msuya,TimesMajira Online,Njombe

KAIMU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ameongoza timu ya Wataalamu ilioundwa kutoka Wizara ya Nishati pamoja Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kukagua eneo litakalojengwa mradi wa kuzalisha Umeme kwa kutumia Maporomoko ya Maji ya Mto Ruhudji.

Muonekano wa sehemu moja ya eneo la Mto Ruhudji ambalo limegawanyika mara mbili katika eneo moja, utakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto huo, lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, Wilayani Njombe Mkoani Njombe.

Timu hiyo iliundwa Mahsusi kwa ajili ya kusimamia kazi za awali kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Ujenzi wa mradi huo, ambapo pia itashirikisha Taasisi na Wizara mbalimbali za serikali.

Ziara hiyo ilifanyika jana ikiwa na lengo la kukagua na kuona Jiografia ya eneo husika lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, Wilayani Njombe Mkoani Njombe.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (kulia) akiteremka mlima kuelekea eneo la Mto, wakati wa Ziara ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ya kukagua na kuona Jiografia ya eneo litakalojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, Wilayani Njombe Mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masanja,mradi huo unatarajiwa kuzalisha takribani Megawati 358 ambazo zitaingizwa katika Gridi ya Taifa pindi mradi huo utakapokamilika.

Katika utekelezaji wa mipango ya Serikali,Mradi huo utaanza kujengwa Mwezi Julai 2021 na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 36.

Mhandisi Masanja, amewatoa hofu Watanzania kuwa endapo mradi huo utalazimika kuchukuwa baadhi ya maeneo ya wakazi wanaozunguka eneo la mradi, sheria na taratibu za nchi zitafuata ili kila mmoja apate haki yake ikiwemo kulipa fidia.

“Mradi huu ni muhimu sana kwetu na umekuja wakati sahihi kwa kuzingatia uchumi wa viwanda, hivyo kuongeza kasi ya uwekezaji katika ujenzi viwanda vipya, kuongeza na kuboresha uzalishaji wa katika viwanda vilivyopo sasa,vilevile kuendelea kutekeleza azma ya serikali ya kuwa na umeme mwingi, wauhakika, wakutosha na wa gharama nafuu nchi nzima”, amesema Mhandisi Masanja.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (kulia) akisaini Kitabu, wakati wa Ziara ya kukagua na kuona Jiografia ya eneo litakalojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa shirika hilo limeupokea mradi huo, na kwamba wako tayari kuanza utekelezaji wa ujenzi wake kulingana na taratibu na miongozo ya Serikali.

Vilevile amesema kwakuwa TANESCO ndiyo msimamizi mkuu wa miradi ya umeme nchini, watahakikisha kuwa wanasimamia vyema utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kunzia hatua za awali na kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati uliopangwa.

“TANESCO tunauzoefu katika kutekeleza miradi Mikubwa na Midogo ya kuzalisha umeme ikiwepo ya Maji, kama vile Mtera, Kidatu, Kihansi na huu mwingine mkubwa kabisa wa Julius Nyerere, pia tuna ile ya Gesi kule Kinyerezi, niwatoe hofu watanzania kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati, na endapo kuna maeneo ya watu katika eneo la kuzunguka mradi sheria na kanuni za nchi zitafuata ili kila mmoja aweze kupata haki yake”, amesisitiza Dkt. Mwinuka.

Ikumbukwe kuwa Januari 8, 2021, Rais Dkt. John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya nje ya China, Wang Yi, ambaye alifanya ziara hapa nchini.

Katika mazungumzo yao pamoja na mambo mengine Rais Dkt.Magufuli aliomba ufadhili kutoka Serikali ya China wa ujenzi wa miradi miwili ya kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maporomoko ya Maji ya Mto Ruhudji na Rumakali.