November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mauaji ya kikatili yatikisa, yanahusisha wazazi, watoto

Na Ashura Jumapili,TimesMajira Online,Bukoba

WATU wawili wamefariki mkoani Kagera katika mauaji ya kikatili yaliyohusisha tukio la baba kudaiwa kumuua mtoto wake kwa kipigo, huku lingine likiwa ni la mama kufariki kwa kunywa sumu. Katika tukio hilo mtoto wa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka mitatu akinusurika kifo baada ya kunyweshwa sumu na mama yake.

Kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili kumethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera jana.

Katika tukio la kwanza Polisi mkoani humo wanamshikilia fundi seremala, Amos Rudovick (39) mkazi wa Kitongoji Mkazaga Kijiji cha Ibale kilichopo Wilayani Kyerwa, mkoani Kagera kwa tuhuma ya mauaji ya mtoto wake, Dustan Amos (13) kwa kipigo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Januari 2, mwaka huu saa tatu usiku.

Kamanda Malimi amesema siku ya tukio marehemu, Dustan ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Ibale, aliondoka nyumbani kwao bila ruhusa ya wazazi wake kwenda kuzurura.

Kwa mujibu wa RPC, mtoto huyo alirudi nyumbani mida ya saa tisa alasiri na alipohojiwa na baba yake alipokuwa, hakuwa na majibu ya kuridhisha.

“Baba yake aliamua kumuadhibu kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani na shingoni na kisha kumuacha bila kumpeleka kupata matibabu,” amesema RPV Malimi.

Amesema mtoto huyo alikutwa na mauti nyumbani akiwa anauguza majeraha ya kipigo cha kikatili kutoka kwa baba yake mzazi ambaye anashikiliwa na Polisi.

Amesema mtoto huyo alizimia na baada ya kuadhibiwa na aliendelea kulala ndani hakutoka hadi ilipofika saa tatu usiku alipogundulika akiwa amefariki.

Amesema uchunguzi wa kitabibu umethibitisha chanzo cha kifo ni majeraha aliyokutwa nayo mwilini ambayo ni pamaoja na kuvunjika uti wa mgongo na shingo.

Amesema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na Polisi na uchunguzi ukikamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Mashtaka ya Taifa kwa ajili ya kuandaa mashtaka na kisha kumfikisha mahakamani mtuhumiwa.

Wakati huo huo, Kamanda Malimi, amethibitisha kutokea kwa tukio lingine la mauaji ya mwanamke anayedaiwa kunywa sumu ya panya na kumnywesha mtoto wake wa miaka mitatu. Mtoto huyo (jina linahifadhiwa) amenusurika kifo.

Amemtaja mwanamke huyo kuwa ni Jesca Samson (37) mkazi wa Kijiji Katoma Ruzinga wilayani Karagwe.

Amesema tukio hilo lilitokea Januari 1, mwaka huu saa sita mchana katika Hospitali ya Nyakahanga Karagwe alikokuwa amelazwa marehemu akipatiwa matibabu na mtoto wake.

Amesema mwanamke huyo aliamua kunywa sumu baada ya mumewe kutoka Magereza alipokuwa amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kuuza kipande cha ardhi bila kumshirikisha.

Alisema taarifa za ushahidi zinadai kwamba wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa kifamilia ambapo mumewe alituhumiwa kwa kosa la kuuza kipande cha ardhi yao bila kumshirikisha mkewe, ndipo aliamua kumshtaki Mahakamani na kuhukumiwa kifungo miezi mitatu gerezani.

Amesema marehemu aliamua kuhama kwa mumewe baada ya kuhukumiwa na kurudi kwa ndugu zake. Amesema akiwa nyumbani kwao aliondoka na ndugu zake wawili kwenda kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2021 Kayanga Mjini baada ya kupokea mwaka majira ya saa nane usiku, walianza safari ya kurudi nyumbani kwao wakiwa njiani akawatoroka na kwenda nyumbani pekee yake na alipofika huko akaamua kunywa sumu ya panya na kumnywesha mtoto wake.

Amesema wenzake walipofika aliwaeleza amekunywa sumu ya panya yeye na mtoto wake, ndipo walipelekwa Hospitali ya Nyakahanga. Kwa mujibu wa RPC alifariki akipatiwa matibabu, huku mtoto wake akiwa amebahatika kunusurika.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kifo cha marehemu ili kufahamu kiini hasa cha kifo hicho.