November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Moyo yaombwa kufikisha uelewa wa magonjwa ya moyo shuleni

Na Mwandishi Maalum,TimesMajira Online,Dodoma

WALIMU wakuu wa shule za Sekondari nchini wameiomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha uelewa wa magonjwa ya moyo unatolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na siyo kwa watu wazima peke yao.

Wamesema uelewa wa magonjwa hayo ukiwafikia wanafunzi utawasaidia kuitunza mioyo yao na hivyo kuweza kuishi maisha marefu zaidi tofauti na inavyofanyika kwa sasa ambapo uelewa unatolewa kwa watu wazima wengi wao wakiwa na umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na baadhi ya walimu waliohudhuria mkutano wa 15 wa walimu wakuu wa shule za sekondari nchini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma.

Walimu hao wamesema ili kuwa na Taifa lenye afya njema ni vyema uelewa ukatolewa kwa makundi yote kwenye jamii wakiwemo vijana walioko shule za msingi na sekondari kwani wao ni wepesi wa kuelewa na kuyafanyia kazi maelekezo wanayopewa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabugaro iliyopo mkoani Kagera, Lucas Kajuna amesema wataalamu wa afya wanajitahidi kuelimisha wananchi lakini bado uelewa wa magonjwa hayo ni mdogo nchini.

“Hasa kwa wengi waishio vijijini ambao hawawezi kupata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, redio na Televisheni,”amesema.

Mwalimu Kajuna ameongeza “Hivi sasa maisha yetu Watanzania wengi yamebadilika tuna magari hata wale ambao hawana wanatumia usafiri wa umma, bodaboda au bajaji, wengi hatufanyi mazoezi hata ya kutembea, tunakula vizuri ila siyo vyakula vyenye afya.

“Je, kutokana na hali hii Watanzania wangapi wanapata uelewa (awareness) wa magonjwa ya moyo ili waweze kuepukana nayo?”, alihoji Mwalimu Kajuna.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnolela iliyopo mkoani Lindi, Adelfina Mbonde,amesema hii ni mara ya pili kushiriki katika mkutano huo na ameshuhudia tofauti kubwa.

“Mkutano wa sasa umekuwa na mada nzuri ikiwemo ya jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo iliyotolewa na Profesa Janabi (Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI) pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa afya,”amesema.

Mwalimu huyo amesema kwa hatua hiyo imewasaidia kupata uelewa jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo kwani mtu anapougua matibabu yake ni gharama kubwa.

“Ninaiomba Serikali itoe uelewa wa magonjwa haya kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi, binafsi nitakaporudi Lindi, nimekusudia kila mwaka kuhakikisha walimu na wanafunzi wa shule ninayoisimamia wanafikishiwa elimu hii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ili wapate uelewa,”amesisitiza.