November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CUF yamuomba Rais Magufuli aanzishe mchakato wa Katiba

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar es Salaam

CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimemuomba Rais John Magufuli kurejesha mchakato wa Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi mapema badala ya kusubiri karibu na uchaguzi mkuu .

Ushauri huo umetolewa Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba katika kongamano la kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya uchaguzi ambalo lilifanyika Makao Makuu ya CUF.

Amesema mchakato wa Tume Huru ya uchaguzi pamoja na katiba mpya unapaswa kuanza mapema badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi mkuu.

Profesa Lipumba amesema kuanza mapema kwa mchakato wa katiba mpya kutasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga umoja kwa wananchi na kurejesha imani kwao.

“Mchakato wa katiba mpya unapaswa kuanza mapema badala ya kusubiri mpaka kipindi cha uchaguzi mkuu, tunamuomba Rais Magufuli hayazingatie haya ili kuepusha yaliotokea katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu,”amesema Profesa Lipumba

Amesisitiza kuwa suala la kukamilika kwa mchakato wa katiba mpya linawezekana hivyo ni muhimu vyama na wadau wote pamoja na Rais John Magufuli kushirikiana ili iweze kupatika Katiba yenye misingi bora.

Ameongeza kurejeshwa kwa mchakato wa katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi kutawaweka Watanzania kuwa pamoja na hatimaye kupata Katiba yenye misingi Demokrasia.

Profesa Lipumba ambaye pia ni mchumi amesema Demokrasia ni nyezo ya maendeleo ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa watu uhuru.

Amesema Dkt.John Magufuli amekuwa akiheshimu misingi ya katiba ikiwemo ukomo wa kuongoza nchi kwa vipindi viwili.

“Rais Magufuli amekuwa akiheshimu mfumo wa kuongoza kwa vipindi viwili hivyo tunamuomba asikubali kushawishiwa na watu na badala yake aendelee kuheshimu utaratibu uliowekwa na katiba mpya,”amesema Profesa Lipumba

Hata hivyo Profesa Lipumba amesema CUF inajikita katika ujenzi wa chama zaidi ili kuweka nguvu katika madai ya kudai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

“Kwa Sasa tupo tayari kushirikiana na watu wengine ikiwemo wadau mbalimbali, vyama vya siasa kwani uwepo wa Tume huru ya uchaguzi na katiba mpya ni muhimu zaidi,”amesema Profesa Lipumba

Kwa upande wake Aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye kwa sasa ni mwanachama wa chama cha Wananchi (CUF )Wilfred Rwakatale amesema chama hicho kinapaswa kuwa mdau namba moja katika kuanzisha mchakato wa katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.