Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dodoma
UONGOZI wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, kupitia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu imemtunukia tuzo ya uongozi Rais Dkt. John Magufuli baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake, ambapo Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli jana kwenye ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, Baba Askofu Dkt. Yohana Masinga iliyofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo Area C Wajenzi jijini Dodoma.
Baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Rais mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na katika hotuba na maelekezo yake kwa viongozi na watendaji wa Serikali amekuwa akisisitiza suala la kumtanguliza Mungu mbele katika kuwahudumia wananchi.
“Ama kwa hakika hofu ya Mungu aliyonayo kiongozi wetu ndiyo hasa siri ya kufanikiwa kwa uongozi wake na Taifa letu kwa ujumla. Sote ni mashuhuda kwamba Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa nchi ya mfano Afrika na Dunia kwa ujumla katika kupiga vita rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma sambamba na kurejesha nidhamu ya kazi ambayo ilikuwa imepotea katika ofisi za umma.”
Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha hivi karibuni dunia nzima imeshuhudia jinsi Tanzania ilivyomtanguliza Mungu wakati wa mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID19).
“Tanzania hatukujifungia ndani kama mataifa mengine. Tuliendelea na shughuli zetu kwa imani kabisa tukijua yupo Mungu ambaye ndiye kinga na msaada wetu pekee,”amesema.
More Stories
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi