October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Ardhi yaanza upimaji ramani,umilikishaji

Na Munir Shemweta, TimesMajira Online,Dodoma

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kazi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika vitongoji 14 vilivyopo Kata ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usanifu Miji na Mipango Kabambe Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Immaculate Senje akizungumza wakati wa mkutano baina ya Timu ya Wizara ya Ardhi na Wananchi wa Chamwino kuhusiana na kuanza kwa zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi katika votongoji 14 vya Kata ya Chamwino mkoani Dodoma.Mpigapicha Wetu

Kazi hiyo imeanza rasmi juzi kwa timu kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani, Elizabeth Mrema kukutana na wananchi wa vitongoji vyote 14 vya Kata ya Chamwino ili kuangalia namna bora ya kuendesha zoezi hilo.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usanifu Miji na Mipango Kabambe Wizara ya Ardhi, Immaculate Senje amewataka wananchi wa vitongoji vya Chamwino kuhakikisha wanamaliza tofauti za migogoro midogo midogo ya ardhi katika maeneo yao kabla ya wataalamu hawajafika uwanjani, ili kurahisisha kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi kwa wananchi.

Amesema iwapo wananchi wa maeneo husika watashindwa kumaliza tofauti zao za migogoro ya ardhi mapema, wataalamu watakapofika watashindwa kuendelea na zoezi mpaka pale utatuzi wa mgogoro utakapomalizika.

‘’Zoezi la upimaji katika eneo la Chamwino hapa Dodoma, linalenga pia kupata maeneo ya miundombinu ikiwemo barabara na zoezi litazingatia njia za awali na kuepuka kugusa nyumba za wananchi,’’ amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani, Elizabeth Mrema aliwatoa hofu wananchi wa maeneo ya vitongoji vya Chamwino kuhusiana na zoezi hilo, ambapo aliwataka kuwapa ushirikiano wataalamu wa Wizara ya Ardhi watakaokuwa wakifanya kazi hiyo.

Amesema hofu ya wananchi kuwa wanaweza kudhulumiwa maeneo yao kupitia zoezi hilo, si za kweli na kusisitiza kuwa Wizara imeamua kuboresha vitongoji vya Kata ya Chamwino, ili kuwawezesha wananchi kuwa na nyaraka za umiliki wa maeneo yao.

Kwa mujibu wa Elizabeth, zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi Chamwino litaanza na vitongoji vitano na baadaye kuendelea na vingine hadi kufikia 14. Alivitaja vitongoji ambavyo zoezi hilo litaanza kuwa ni Sokoine, Ukombozi, Kambarage, Umoja na Azimio.

Kwa upande wake Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Letare Shoo aliwaambia wananchi wa wilaya hiyo kuwa kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji maeneo katika vitongoji vya Chamwino, umegawanyika kwenye makundi makuu mawili aliyoyaeleza kuwa ni urasimishaji au uboreshaji maeneo yaliyojengwa bila kufuata taratibu na pili ni kupima mashamba makubwa kwa kuanisha matumizi yake ikiwemo viwanja.

Hata hivyo Ofisa Ardhi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino alisema, tofauti na maeneo mengine ambapo wananchi wa Chamwino watapata unafuu katika gharama wakati wa zoezi hilo, badala ya kulipia 150,000 wao watalipia sh. 50,000 kwa kila kiwanja.

‘’Halmashauri ya Manispaa ya Chamwino ina jumla ya vijiji 107, lakini Kijiji cha Chamwino kimepata upendeleo wa kipekee kupimiwa na wataalamu wa Wizara ya Ardhi,’’ amesema.

Mmoja wa wananchi wa Kitongoji cha Talama katika Kata ya Chamwino, Dikson Mchiwa mbali na kuipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wa kupanga, kupima na kumilikisha maeneo Chamwino alitaka wizara kuhakikisha zoezi hilo, linatakelezwa hasa ikizingatiwa kumekuwa na kigeugeua cha kuelezwa upimaji utafanyika halafu haufanyiki.