Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
KATIBU wa Bunge, Steven Kagaigai ametangaza kuanza kwa Bunge la 12 Novemba 10 mwaka huu jijini Dodoma huku akiwataka wabunge wa kuchaguliwa na kuteuliwa kufika katika Ofisi za Bunge wakiwa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kujisajili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Kagaigai amesema usajili wa wabunge unaanza leo Novemba 7 hadi 9 mwaka huu katika ofisi za Bunge jijini Dodoma ambapo amewataka wabunge kufika na nyaraka mbalimbali.
Amezitaja nyaraka hizo kuwa ni pamoja na Hati ya kuchaguliwa au kuteuliwa, nakala ya kitambulisho cha NIDA, Kadi ya benki ya Mbunge na cheti cha ndoa kinachotambuliwa na serikali.
Amezitaja nyaraka nyingine kuwa ni vyeti vya kuzaliwa vya watoto walio chini ya umri wa miaka 18, vyeti vya elimu ya Mbunge ambavyo husaidia namna ya kuwapanga wabunge katika Kamati za Bunge pamoja na picha ndogo (passport size) nane .
Aidha Katibu huyo wa Bunge amesema shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha bunge, uchaguzi wa Spika, kiapo cha umainifu kwa wabunge wote, kuthibitisha jina la Waziri Mkuu, uchaguzi wa Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania